Habari

Tanzania
Waziri Simbachawene Awaonya Wananchi Wanaoharibu Vyanzo Vya Maji Jimboni Kibakwe Dodoma - Tanzania

JULAI 21, 2023
Border

Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Jijini Dodoma ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini Tanzania Mhe.George Simbachawene ametoa ovyo kwa wananchi wanaoharibu vyanzo vya maji huku akiutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoni Dodoma kusimamia ipasavyo zoezi hilo.

Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika Vijiji cha Chang’ombe na Kidenge vilivyopo katika Kata ya Luhundwa, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma kupitia mikutano ya hadhara ya Mbunge huyo katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, ikiwa ni muendelezo wa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama chake Cha Mapinduzi.

Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo kufuatia mwananchi mmoja kufanya shughuli za kilimo na ufugaji katika chanzo cha maji cha Igombo.

Amesema chanzo cha maji cha Igombo ni muhimu sana kwa mustakabali wa maisha ya wananchi wa Luhundwa na Kibakwe kwa ujumla hivyo kikiharibiwa kutakuwa na athari kubwa.

Mhe. Simbachawene ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kumuondoa mara moja mwananchi huyo ili kunusuru chanzo hicho cha maji ambacho ni muhimu na tegemeo kwa wakazi wa maeneo hayo.

‘‘Maji ni uhai, siko tayari kuona vyanzo vya maji vikiharibiwa kwa maslahi ya watu wachache, ni lazima tuchukue hatua ili iwe funzo kwa wengine” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Amesema athari za uharibifu wa mazingira zinagusa moja kwa moja masilahi ya wananchi wote bila kujali wewe ni nani katika jamii.

Oliver G Nyeriga - MTV TANZANIA