Tanzania

Wananchi Wanufaika Na Ujenzi Na Ukarabati Wa Barabara Tanzania - Mhe. Ndejembi

JULAI 24, 2023
Border
news image

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbiga watanufaika na ujenzi pamoja na ukarabati barabara unaofanywa na Serikali kupitia fedha za Mradi wa Uboreshaji Miundombinu katika Miji (TACTIC), AGRI-CONNECT na zilizotengwa kwenye bajeti ya TARURA.

Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa katika Halmashauri ya Mji Mbinga, mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi wa Mbinga.

Mhe. Ndejembi amesema, kupitia mradi wa TACTIC usanifu wa kujenga barabara za lami 12 katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga utakamilika muda si mrefu na mkandarasi ataanza ujenzi, na kuongeza kuwa kupitia mradi huo Mbinga itajengewa soko la kisasa.

Mhe. Ndejembi ameainisha kuwa, kupitia mradi wa AGRI-CONNECT barababara nyingine ya Luwaita yenye urefu wa kilomita 15.7 ambayo usanifu wake umeshakamilika, imewekwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka huu wa fedha 2023/24.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema, ipo barabara inayotoka Mbinga kwenda Mpepai na Liparamba yenye urefu wa Kilomita 41.87 ambayo imetengewa milioni 400 katika mwaka huu wa fedha 2023/24 kwa ajili ya kutengeneza maeneo korofi ili iweze kutumika wakati wote.

“Mhe. Makamu wa Rais, ninawahakikishia wananchi wa Mbiga kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko kazini kuwaboreshea miundombinu ya barabara ambayo ni chachu ya maendeleo katika taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Sanjari na hilo, Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa ndani kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita, bajeti ya TARURA kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga iliongezwa kutoka milioni 930 hadi bilioni 2.2, na katika mwaka huu wa fedha TARURA imetengewa zaidi ya bilioni 2.9 kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizopo katika halmashauri hiyo ya mji.

Oliver G Nyeriga