TANZANIA

Upatikanaji Wa Huduma Ya Maji Kuongezeka Dodoma Tanzania

JULAI 30, 2023
Border
news image

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) nchini Tanzania Mhandisi Aron Joseph amesema muda wa upatikanaji wa huduma ya Maji kwa wakazi wa Dodoma utaongezeka kutoka saa 13 hadi 19 kwa siku mwishoni mwa mwaka 2024 baada ya kukamilika kwa miradi minne ya muda mfupi ya uchimbaji wa visima inayogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 30.7

Aidha mahitaji halisi ya Maji kwa Jiji la Dodoma ambalo ndio makao makuu ya nchi ni lita milioni 133.4 kwa siku huku uzalishaji ukiwa ni lita milioni 68.6 hivyo upungufu uliopo ni lita milioni 64.8 hali inayoilazimu Mamlaka ya DUWASA kuwa na mipango ya muda mfupi, kati na mrefu.

Mhandisi Aron ameainisha mpango huo wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma.

"Lengo la mpango huu ni kupunguza adha kwa wakazi katika maeneo hayo, na kupunguza utegemezi wa chanzo kikubwa cha Mzakwe, wakati tunasubiri uwekezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati jijini Dodoma"

Pia Mhandisi Aron Ameeleza mkakati wa kuboresha Miundombinu ya Maji taka katika kata zote za Jiji la Dodoma

"Kwa kushirikiana na Wizara ya Maji inatekeleza mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa maji mjini Dodoma na kuondosha majitaka Mipango hii imegawanyika katika sehemu kuu zifuatazo, Muda mfupi, Muda wa Kati, Muda mrefu na Mpango wa Dharula/haraka"

"Katika mpango wa muda mfupi, DUWASA inaendelea na utafiti, kuchimba na kuendeleza visima maeneo ya pembezoni mwa mji lengo la mpango huu ni kupunguza adha kwa wakazi katika maeneo hayo, na kupunguza utegemezi wa chanzo kikubwa cha Mzakwe, wakati tunasubiri uwekezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati jijini Dodoma" amesema Mhandisi Aron

Oliver G Nyeriga - MTV TANZANIA