Shirika la Reli Tanzania TRC linaendelea na majaribio ya mifumo ya vifaa vya uendeji wa Reli ya kisasa SGR vinavyotengenezwa na Kampuni ya Hyundai Rotem katika mji wa Changwon, nchini Korea ya Kusini, Julai, 2023.
Kampuni ya Hyundai Rotem ilipewa tenda ya kutengeneza vichwa 17 vya treni vya umeme Pamoja na seti 10 za treni za Kisasa za EMU maarufu kama “Treni zilizochongoka”.
Timu ya wataalamu kutoka TRC Tanzania inayoundwa na Wahandisi mitambo, wahandisi umeme, mafundi na madereva wa Treni imeweka kambi katika kiwanda cha Hyundai Rotem kwaajili ya ukaguzi wa mifumo mbalimbali ikiwemo umeme, mfumo wa breki na vipimo katika utengenezaji wa vichwa vya treni vya umeme.
Kiongozi wa Timu hiyo ya wataalamu ambae pia ni meneja wa mradi wa ununuzi wa vifaa vya uendeshaji vinavyotengenezwa na Kampuni ya Hyundai Rotem, Mhandisi Kelvin Kimario ameeleza kuwa zoezi la ukaguzi wa kiwandani ni muhimu ili kujiridhisha kuwa vifaa vilivyotengenezwa vimefuata masharti ya mkataba na viwango vya reli iliyojengwa.
“bila kufanya ukaguzi wa kiwandani, kifaa kinaweza kusafirishwa na baanda ya kufika nchini unagundua hakifanyi kazi iliyokusudiwa, au vipimo vyake haviendani na miundombinu kama vile madaraja na mahandaki tuliyojenga, na matokeo yake kuisababishia serikali hasara au kuhatarisha usalama wa miundombinu na watumiaji” alisema Mhandisi Kimario.
Watengenezaji wa vichwa vya treni vya umeme kampuni ya Hyundai Rotem wanaeleza kuwa vichwa hivyo 17 vya umeme vyenye uzito wa tani 88 kila kimoja vimetengenezwa kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania, aidha kampuni hiyo imeeleza kuyapa kipaumbele mafunzo kwa madereva na mafundi kutoka TRC ili kuwajengea uwezo katika teknolojia hiyo mpya inayotegemewa kuleta mapinduzi katika usafirishaji kwa njia ya reli nchini Tanzania.
“Tumechukua kiwango cha wastani cha mvua cha dar es salaam ambacho ni milimita 254…lakini hapa tumekizidisha mara nne na tunayaruhusu maji haya kwa dakika 15 na baada ya hapo tunasubiri kwa dakika 10 kabla ya kukagua eneo moja hadi jingine hii ni kuhakikisha hakuna uwezekano wa maji kuathiri mfumo wa umeme na vifaa vyake ndani ya kichwa” aliongeza Meneja mradi wa utengenezaji wa vifaa hivyo Bwana Sangho Lee wakati wa jaribio la uwezo wa vichwa hivyo kutopitisha maji wakati wa mvua.
Kwa upande wao mafundi na madereva wa treni walioshiriki katika majaribio hayo yatakayoendelea kwa juma zima nchini Korea ya Kusini, wameeleza kuwa kushiriki katika zoezi hili muhimu kutawasaidia kuvifahamu vizuri vifaa hivyo na kuutumia ujuzi huo vifaa hivyo vitakapoanza kufanya kazi nchini.
Zoezi la ukaguzi wa vichwa vya treni vya umeme ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, juu ya kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya uendeshaji wa Reli ya Kisasa SGR, Pamoja na kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa nchini.