TANZANIA

Tume Ya Umwagiliaji Tanzania Yatekeleza Bajeti Ya 2022 - 2023 Kwa Asilimia 100

JULAI 30, 2023
Border
news image

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Tanzania Bw.Raymond Mndolwa amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji kwa kuelekeza bajeti kubwa katika sekta hiyo ya Shilingi Bilioni 361.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mndolwa ameyasema hayo wakati wa kuelezea utekelezaji wa bajeti ya Taasisi yake kwa mwaka 2022-2023 kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambapo utekelezaji wa bajeti hiyo umefikia asilimia 100%.

"Kwa mara ya kwanza sekta hii ya kilimo tumepata fedha nyingi sana kwa mwaka 2022-2023. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilipewa bajeti ya Shilingi Bilioni 361 kwaajili ya kutengeneza skimu mpya 25, kufanya ukarabati wa Skimu 30, kusanifu miradi 42 ya skimu nchi nzima, kazi hiyo imefanyika Kwa asilimia 100%.

Miradi mingine iloyotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ni pamoja na uchimbaji wa Mabwawa 14 ya kuvuna maji kuwawezesha wakulima walime zaidi ya mara moja.

Aidha Mndolwa amesema kuwa katika bajeti ya mwaka 2023-2024 serikali imeelekeza Shilingi Bilioni 373, fedha hizo zitatumika kumalizia miradi inayoendelea kujengwa, miradi 25 mipya, miradi 30 ya ukarabati na miradi 42 ya usanifu.

Aidha kupitia bajeti ya 2023-2024 Tume ya Taifa ya umwagiliaji itawekeza kwa wakulima wadogo wadogo kwa kuchimba zaidi ya visima 1,845 katika halmashauri zote 184 ambapo wakulima 150 Kila halmashauri watafungiwa mfumo wa umwagiliaji ili kila mkulima aweze kuzalisha kwenye hekari zake mbili na nusu kwa lengo la kuongeza tija ya kilimo Cha umwagiliaji miongoni mwa jamii.

Aidha ili kuongeza ufanisi zaidi, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inahamasisha sekta binafsi kilimo cha mashamba makubwa (Block Farm) kwaajili ya vijana na akina mama katika mikoa ya Kigoma, Njombe, Mbeya, Kagera na Dodoma kupitia programu ya Build Better Tomorrow.

Mndolwa pia amesema Tume ipo mbioni kutumia mfumo wa kidijitali kuwatambua wadau wa kilimo ambapo maafisa wa Tume katika skimu za Umwagiliaji watatumia Vishikwambi kwaajili ya kuratibu zoezi hilo.

Mkurugenzi Mndolwa ametumia fursa hiyo kuwasihi wakulima katika sekta ya Umwagiliaji kuchangia ada ya huduma za umwagiliaji kwakuwa ndio inayosaidia shughuli za ukarabati wa skimu zinapoharibika na kwamba hatua za ukarabati hugharimu fedha nyingi.

Oliver G Nyeriga - MTV TANZANIA