Tanzania

Tshs. Milioni 5 Kupata Kibali Cha Kumpa Mnyama Jina Lako Tanzania

JULAI 24, 2023
Border
news image

Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania kupitia Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) William Mwakilema amesema kuanzia mwaka huu 2023 wameanzisha programu maalum ya mtu anayetaka kuasili ama kumpa mnyama jina lake anaweza kufanya hivyo lakini kwa kulipia fedha za kitanzania Milioni 5 fedha ambayo itatolewa na mwenye jina ili apate kibali cha kumpa jina mnyama.

Hilo limekuja baada yakuonekana baadhi ya majina ya binadamu wanayopewa wanyama kuvutia watu wengi hali ambayo imewasukuma mamlaka hiyo kuanzisha utaratibu huo na fedha zitakazopatikana zinakwenda kuendesha shughuli za utunzaji za wanyamapori na uhifadhi mali asili ya nchi.

Kamishna muhifadhi TANAPA Mwakilema ameyabainisha hayo leo Jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu yao na mwelekeo wa utekelezaji wa mipango kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Amesema "tumeanzisha utaratibu wa kuwapa majina baadhi ya wanyama lakini sio bure na hao wanyama sio wote labda kama umesema kuwa unampenda sana Fisi unataka huyo fisi awe na jina lako atapewa kwa utaratibu maalum,”amesema Mwakilema

Amesema bodi ya menejimenti ya TANAPA imeshapitisha utaratibu huo ambao utaanza na wanyama aina ya Faru.

Pia amesema mtu yoyote anaweza kufanya hivyo kama anataka hivyo ataenda kumuona mnyama husika na anaweza kumuasili na atatakiwa kuchangia gharama za kumuhifadhi mbugani Shilingi Milioni 1 kila mwaka.

Hata hivyo, amesema wapo baadhi ya Faru pia wana majina akiwemo yeye mwenyewe ambaye mmoja wa faru katika Hifadhi ya Serengeti amepewa jina lake.

Aelezea asili ya Bob junior huku akisema Simba aliyepewa jina la Bob Juniour, Kamishna Mwakilema amesema jina hilo alipewa na waongoza utalii baada ya kulinganisha mnyama huyo wakamlinganisha na Bob Marley ambaye alivyokuwa na Rasta zake nyingi, ukubwa na kivutio kwa watalii.



“Bahati mbaya jina hilo halikutambulika hadi alipokuja kufa akaanza kuvuma kuwa Bob Junior amekufa,”amesema kamishna Mwakilema.

Amesema bodi ya menejimenti ya TANAPA imeshapitisha utaratibu huo maalum ambao utaanza na wanyama aina ya Faru na baada ya baadhi ya wanyama waliopewa majina ya watu maarufu wa nje ya nchi na ndani ya nchi na kuonekana kupendwa na kuwa kivutio ni pamoja na Simba Bob Juniour, Faru John na Faru Rajabu.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania