Habari

Tanzania
BBT Programu Yaanza Kuzaa Matunda Tanzania

JULAI 19, 2023
Border

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Mhe.Hussein Bashe amewapongeza vijana wanaonufaika na programu ya Wizara ya Building a Better Tomorrow (BBT) kwa kuanza kuvuna na kuuza mazao waliyozalisha kwenye kituo atamizi cha Bihawana, jijini Dodoma.

Akizungumza na baadhi ya vijana hao waliomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma, na kutoa shukrani na kumuonesha bidhaa walizozalisha, Mhe. Bashe amesema amefurahishwa sana na matokeo aliyoyaona ya utayari wa vijana wa BBT.

Waziri Bashe ameendelea kuwatia moyo vijana hao kutanua wigo wa kusambaz mavuno yao kwenye maeneo mbalimbali jijini Dodoma, zikiwemo ofisi za Umma ili kukidhi hitajio la mazao hayo kwa walaji.

Mmoja wa wanufaika wa programu ya BBT, Bi. Asia Msuya amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhamasisha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo kwani kilimo ni biashara.

Bi. Msuya ameeleza kuwa kupitia programu ya BBT, amepata maarifa ya kilimo na sasa yupo tayari kufanya shughuli za kilimo kwa weledi na kujipatia kipato.

Naye Bw. Razaki Mbaraka wa BBT amesema wameanza zoezi la kufikisha mazao yao wenyewe moja kwa moja kwa walaji, hatua inayowawezesha kuuza kwa faida na kuepuka usumbufu wa madalali.

Bw. Mbaraka amesema kuwa kuuza mazao yao pasipo kupitia kwa madalali imekuwa chachu ya kupata kipato kwa haraka zaidi kutokana na maarifa waliyopatiwa kuhusu Biashara ya Kilimo yanayowasaidia kutatua changamoto za madalali na kujiongezea kipato.

Aidha, Bw. Mbaraka amemshukuru Waziri Bashe kwa kuzidi kutoa hamasa kwa vijana wa BBT ambao wanaanza kuona matunda ya programu hiyo kibiashara.

Oliver G Nyeriga -MTV TANZANIA