Habari

TANAPA Yajipanga Kuongeza Idadi Ya Watalii Tanzania

JULAI 24, 2023
Border
news image

Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA limejipanga kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 343.8 katika mwaka wa fedha 2023/2024 tofauti na mwaka jana ambapo ilikusanya shilingi bilioni 337.

Akitoa taarifa hiyo Julai 24, 2023 katika mkutano na wanahabari ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari - Maelezo jijini Dodoma juu ya mwelekeo wa Shirika hilo katika kukuza shughuli za Utalii kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Kamishna Mwakilema amesema "TANAPA imeweka mikakati thabiti ya kuongeza idadi ya watalii kufikia 1,802,460 kwa mwaka 2023/2024".

Kamishna Mwakilema alisema, "shirika lina dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoteuliwa kuwa hifadhi za taifa hivyo TANAPA imeweka vipaumbele katika maeneo ya uhifadhi, ulinzi, utalii, ushirikishaji jamii na uboreshaji wa miundombinu pamoja na ukamilishaji wa miradi ya kimaendeleo ya shirika ili kufikia malengo tuliojiwekea".

Aidha, shirika limejipanga kuboresha miradi ya maendeleo kwa ukarabati wa viwanja vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi na Nyerere, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege na Helikopta ili kuimarisha utalii pamoja na shughuli za ulinzi mkakati.Hata hivyo, Kamishna Mwakilema alisema, "shirika limeendelea kujipanga katika kuboresha miradi ya maendeleo kwa kutenga bilioni 60.6 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuwezesha utekelezaji wa maendeleo katika miradi mbalimbali inayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA)".

Sanjari na utekelezaji wa mipango hiyo itakayoweza kuimarisha uchumi kwa shirika na taifa kwa ujumla TANAPA pia, imejipanga kumaliza changamoto za uhifadhi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za uhifadhi na serikali kwa kufanya kazi kwa weledi ili kumaliza migogoro ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alitoa shukrani kwa shirika kutoa ufafanuzi juu ya muelekeo wa TANAPA mbele ya wanahabari hao ambao utawaongezea uelewa kutoa taarifa sahihi zinazohusiana na ulinzi wa hifadhi za taifa na kuwa mabalozi wazuri wa kuvitangaza vivutio vya utalii kwa wananchi na namna shirika hilo linavyofanya kazi zake kwa weledi na maarifa.

"Nikushukuru sana Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA kwa taarifa yako yenye malengo chanya ya kukuza utalii na iliyotilia mkazo suala zima la uhifadhi wa maliasili. Hivyo ni matumaini yangu kuwa wanahabari hawa wameelewa dhana nzima ya uhifadhi wa vyanzo vya maji hivyo kupitia kalamu zenu watanzania wataelewa shughuli nzima ya uhifadhi"- alisema Msigwa.


Aidha, shirika linaendelea kutekeleza sera ya ujirani mwema ambapo pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi shirika litaendelea kutekeleza miradi ya ujirani mwema iliyoanzishwa na jamii kwa kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 2.3 kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, katika wilaya 20 za kipaombele.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania