Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kutumia tafiti mbalimbali zinazofanyika kwa lengo la kuwa na afua na mikakati itakayosaidia kuondokana na vitendo vya ukatili hasusan dhidi ya Watoto na Vijana nchini.
Hayo yamebainika jijini Dodoma Julai 24, 2023 katika kikao kazi cha kujadili utafiti kuhusu Ustawi, Afya ya Watoto na vijana kilichowakutanisha Makatibu wakuu kutoka Wizara za kisekta Tanzania Bara na Zanzibar.
Akiongoza kikao kazi hicho Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Wakili Amon Mpanju amesema, kikaokazi hicho kimelenga kuangalia namna bora ya kuwa na mikakati ya kufanya tafiti itakayo saidia kutatua suala la ukatili na mmonyoko wa maadili nchini.
Mpanju amesema utafiti huo ni muhimu kwa mstakabali wa Ustawi wa Watoto na Vijana wa kitanzania na ni nyezo muhimu ili kuhakikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweka mifumo mizuri ya ulinzi na usalama wa watoto na vijana.
"Tumeamua kufanya utafiti huu ili iweze kutupa matokeo na kutusaidia kupata afua za kupambana na ukatili dhidi ya ukatili wa watoto na vijana katika jamii hasa kupata viwango aina na madhara ya ukatili ndani hamii" alisema Wakili Mpanju
Amesisitiza kuwa utafiti huo itasaidia kung'amua masuala mbalimbali ambayo yamechangia uwepo wa ukatili ili kisaidia Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na afua nzuri za kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Akieleza mikakati mbalimbali ya Serikali katika kupambana na ukatili nchini ni uwepo wa Mpango wa Kitaifa wa kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, Madawati ya Jinsia katika Jeshi la Polisi, Magereza, Taasisi za Serikali, maeneo ya umma, Madawati ya Watoto Shuleni na mikakati mbalimbali ya kupambana na tatizo hilo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Zanzibar Siti Abbas Ali akitoa maelezo wakati wa kikao kazi amesema utafiti huo utasaidia pia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar kuwa na afua mbalimbali zitakazosaidia Serikali kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii hasa kwa watoto na vijana vinavyoathiri kundi hilo ambalo ni muhimu katika Ustawi wa Taifa lolote duniani.Akiwasilisha muhtasari wa utafiti tarajiwa wakati wa kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) Dkt. Redemta Mbatia amesema kuwa utafiti wa UNICEF kuhusu masuala ya ukatili unaonesha kuwa watoto Billioni 1 kati ya umri wa miaka 2-17 walikuwa wamefanyiwa ukatili wa kimwili kingono na kisaikolojia katika Kipindi cha mwaka mmoja 2022 hivyo ni muhimu kufanya utafiti utakaosaidia kupata mikakati mbalimbali ya kupambana na vitendo hivyo katika jamii.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia na masuala ya watoto (UNICEF) John George amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha utafiti huo unafanikiwa ili kuwezesha kufanya shughuli zao hasa katika kupambana na ukatili dhidi ya Watoto Duniani hasa katika kuweka Mipango, Sera, Miongozo na Sheria za kumlinda dhidi ya vitendo vya ukatili.
"Na sisi kama Shirika utafiti huo utatusaidia kupata taarifa ambazo zitatuwezesha kuweka Mipango na mikakati katika kutekeleza shughuli mbalimbali zinazohusu afua za watoto hasa katika kupambana na vitendo vya ukatili hasa dhidi ya watoto" alisema John
Akichangia katika kikaokazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo amesema ni muhimu kuangalia pili upande wa kesi za ukatili dhidi ya Watoto na namna gani Taasisi mbalimbali za Serikali na wadau watashirikiana katika kuhakikisha kesi za ukatili zinasimamiwa vyema na kuhakikisha wahanga wa vitendo hivyo wanalindwa na watuhumiwa wanafikishwa katika vyombo vya Sheria.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa Kitaifa na kimataifa wanashirikiana katika kufanya utafiti kuhusu Ustawi, Afya ya Watoto na vijana utakaosaidia kutatua changamoto za vitendo vya ukatili hasa dhidi ya Watoto na Vijana.