Tanzania

Serikali Ya Tanzania Kutoa Milioni 500 Kwa Ajili Ya Ujenzi Wa Kituo Cha Afya Peramiho - Mhe. Ndejembi

JULAI 24, 2023
Border
news image

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Mhe. Angellah Kairuki ameahidi kuwa Serikali itatoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Peramiho ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoyatoa mara baada ya Mbunge wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama kuwasilisha ombi la kujengewa kituo cha afya.

Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Peramiho kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki, mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango kumpatia fursa ya kuzungumza na wananchi hao.

Mhe. Ndejembi amesema kwa heshima na maelekezo ya Makamu wa Rais, fedha hiyo itatolewa mapema iwezekanavyo ili kuwezesha ujenzi wa kituo cha afya ambacho kitaboresha utoaji wa huduma za afya kwa jamii.

“Ujenzi wa kituo hicho unatokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Peramiho Mhe. Jenista Mhagama ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni ataleta gari mbili za kubebea wagonjwa katika Halmashuri ya Wilaya ya Songea, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa maboresho ya utoaji wa huduma za afya katika Hamashauri hiyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa mafanikio ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilayani Songea na katika maeneo mengine yanajianisha wazi kupitia kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya elimu ya awali, msingi na sekondari.

Oliver G Nyeriga - MTV TANZANIA