Habari

Tanzania
Rais Wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Kuweka Jiwe La Msingi Ujenzi Wa Mnara Wa Mashujaa

JULAI 24, 2023
Border
news image

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Rais , Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Mnara wa Mashujaa unaojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa yatakayofanyika kesho Julai 25 mwaka huu Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika Mikoa na Wilaya zote nchini kwa kufanya shughuli za Kijamii kama vile kupanda Miti, kufanya usafi wa mazingira ya kijamii na kufanya Kumbukumbu ya Mashujaa kwa Mikoa na Wilaya ambayo ina Minara au Makaburi ya Mashujaa.

“Katika kukuza Uzalendo kwa Wananchi nchini, Maadhimisho haya ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa Mwaka huu 2023 yatafanyika katika uwanja huu kwa mara ya kwanza ikiwa ni maagizo ya Mheshimiwa Rais ambapo aliagiza kujengwa kwa mnara wenye hadhi ya makao makuu ya Nchi hatua inayoonyesha nia njema ya Mheshimiwa Rais anavyojali, kuithamini na kuilinda hazina ya historia ya nchi yetu,” Amesema Mhe. Jenista.

Pia Mhe. Jenista amebainisha kuwa Shughuli za Maadhimisho hayo ni pamoja na Gwaride la maombolezo, uwekaji wa Silaha za asili na Maua kwenye Mnara wa Mashujaa pamoja na Dua na Sala kutoka kwa Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini nchini.

“Naomba nichukue fursa hii kuwaomba Wanahabari wote kuendelea kuhamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu katika Kumbukumbu hizi muhimu kwa historia ya nchi yetu na pia kuendelea kuwa Wazalendo na kutunza Tunu za nchi yetu Amani na Utulivu,” Ameeleza.

Katika hatua nyingine amefafanua hatua ya ujenzi wa Mnara na Uwanja wa Mashujaa akisema kwamba umekamilika kwa hatua ya kwanza kwa kujenga Uwanja wa Mashujaa utakaokuwa unatumika kwa Gwaride la vyombo vya Ulinzi na Usalama na matukio na shughuli zingine za Serikali.

“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kupitia Mkandarasi SUMA JKT na Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Ardhi (ABECC) wanaendelea kukamilisha awamu ya kwanza ya Ujenzi wa Mnara wa kudumu wa Mashujaa ambapo wameishamaliza kujenga. Aidha, ujenzi wa Mnara wa kudumu unaendelea kujengwa na upo katika hatua nzuri,” Ameeleza Mhe. Jenista.

Aidha amewahimiza watanzania na wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili kuwa sehemu ya historia ya nchi katika kumbukumbu ya Mashujaa waliojitolea kupigania Taifa ambapo mpaka sasa limeendelea kuwa sehemu salama na uwepo utulivu na Amani.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mhe. Innocent Lugha Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Rais , Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi ya ujenzi wa Mnara huo na kuahidi kama wizar kutoa ushirikiano katika hatua zote za ujenzi hadi kukamilika kwake.

Oliver G Nyeriga