Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kutumia vema rasilimali ya Ziwa Nyasa ambalo lipo katika eneo lao ili kuwa na matumizi endelevu kiuchumi na kijamii

JULAI 24, 2023
Border
news image

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 23 Julai 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Mbambabay akiwa ziarani mkoani Ruvuma. Amesema vitendo vya utupaji taka za plastiki katika ziwa hilo vitaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uvuvi kwani taka za platiki huchukua miaka mingi zaidi kuoza na kutoweka.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi hao kutunza vyanzo vya maji pamoja na kulinda mazingira kwa jitihada kubwa. Amesema serikali katika mwaka wa fedha 2023-2024 tayari imetenga fedha za ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa Kimbande utakaonufaisha wananchi wa Wilaya hiyo.

Vilevile Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Nyasa kujitokeza na kutumia vema fursa ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaig) iliozinduliwa mkoani Ruvuma ili kupata msaada wa kisheria katika changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo mirathi.

Pia amewataka wananchi wa Mbambabay kulinda amani iliopo nchini kwa kuwa makini na watu wote wanaohatarisha amani wanaoingia kupitia mipaka yae neo hilo. Aidha amewasihi wazazi na walezi kusimamia maadili na uzalendo kwa watoto na vijana ili kuwa na Taifa salama kwa sasa na baadae.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema serikali tayari imetenga shilingi bilioni 22 kujenga Daraja la Mitomoni lilikuwa changamoto kwa muda mrefu iliopelekea wananchi kuzunguka umbali mrefu kufika Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma. Pia amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa Barabara ya Likuyufusi – Mkenda ambapo kwa hatua ya awali ni ujenzi wa kilometa 60 kwa kiwango cha lami Likuyufusi – Muhukulu.

Awali Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameweka Jiwe la Msingi Mradi wa maji wa Liuli uliopo Kijiji cha Hongi Wilaya ya Nyasa, mradi uliogharimu shilingi bilioni 4.7 unaohudumia vijiji vitano vyenye wakazi 15,823.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa eneo hilo kulinda miundombinu ya maji ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu. Pia ameagiza ziada ya maji inayopatikana kutokana na mradi huo ambayo imekua ikirudishwa ziwani kutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.