Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema taasisi za kifedha za kikanda na kimataifa zinapaswa kujishughulisha zaidi katika kubuni na kutoa masuluhisho ya kifedha ili kuunga mkono azma ya nchi za Afrika ya kuharakisha maendeleo ya rasilimali watu.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia viongozi mbalimbali wa Afrika akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufunguzi wa Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam. Amesema uwekezaji katika Rasilimali watu ni wa muda mrefu hivyo unahitaji ufadhili wa gharama nafuu kutoka taasisi hizo za fedha za kimataifa.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi za mafunzo na elimu kuhakikisha zinasaidia bara la Afrika kuimarisha uwezo wa wazawa katika kusimamia na kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo. Amesema Bara la Afrika linatumia rasilimali nyingi za kifedha katika kutafuta maarifa na rasilimali watu kutoka nje ya bara hilo kwa ajili ya kutumia maliasili zilizopo. Ameongeza kwamba kutokana na umuhimu wake taasisi za mafunzo barani Afrika zinapaswa kushirikiana na kutafuta suluhisho ya changamoto zinazolikabili bara hili.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa mkutano huo kutafuta njia bora zaidi ya kuihamasisha sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuzalisha rasilimali watu iliyo bora kwa kuwa sekta binafsi ni wanufaika wakubwa wa maendeleo ya rasilimali watu.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Bara la Afrika na Wadau wa maendeleo kuwekeza zaidi katika Elimu, Afya, Lishe, Maendeleo jumuishi pamoja na ulinzi wa jamii. Ametoa wito kwa wahudhuriaji wa mkutano huo kujadili na kupata sera za kibunifu zitakazosaidia katika kuboresha maendeleo ya rasilimali watu na kuwapa uwezo idadi kubwa ya vijana inayoongezeka barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha inaboresha rasilimali watu kwa kuwekeza katika sekta za elimu, afya na kilimo ikiwemo kuongeza bajeti na kuhakikisha miundombinu rafiki katika sekta hizo. Amesema hatua zilizochukuliwa zimesaidia katika kupata matokeo chanya ikiwemo ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule kutoka asilimia 85 mwaka 2015 hadi 97 mwaka 2021 huku kiwango cha wanaohitimu elimu ya msingi kufikia asilimia 100 mwaka 2022 kutoka asilimia 80 mwaka 2015. Ameongeza kwamba vyuo vya ufundi nchini Tanzania vimejengwa katika mikoa 30 kati ya 31 pamoja na kuongezeka kwa uwiano wa kijinsia wa 1:1 katika kupata elimu.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema Tanzania inapitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Sheria ya Elimu na Mitaala mapitio yanayolenga kuboresha mfumo wa elimu ili kukidhi ukuzaji wa vipaji, ujuzi wa vitendo, umahiri wa kujenga, fikra chanya na kuwafanya wahitimu kutambua teknolojia ya hali ya juu. Amesema jambo hilo linatarajiwa kuongeza tija kwa vijana, ushindani katika soko la ajira pamoja na kuwaandaa wahitimu kuwa wabunifu wa kazi kwa kujiajiri zaidi kuliko kuajiriwa.
Pia amesema katika jitihada za kuimarisha rasilimali watu juhudi zinaelekezwa katika utoaji wa mafunzo, mapinduzi ya kidijitali, kuongeza utoaji wa huduma za jamii pamoja na usambazaji wa nishati ya umeme ili kufikia vijiji vyote. Vilevile, kuimarisha miundombinu ya TEHAMA kwa kutambua ongezeko la wanaotumia intaneti kutoka asilimia 36.5 mwaka 2015 hadi asilimia 49 mwaka 2021.