Tanzania

Kinana: Usikivu Wa Rais Dk. Samia Nchi Imetulia

JULAI 24, 2023
Border
news image

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Tanzania Bara Abdulrahaman Kinana,amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ndani ya kipindi cha miaka miwili kutokana na uongozi wake mzuri unatokana utulivu,usikivu,kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania.

Kinana ameyasema hayo jana wilayani Kondoa mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Dk.Ashatu Kijaji kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka miwili na nusu chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia.

“Kwa hali ilivyo na kwa hatua tuliyopiga tukienda hivi tunavyokwenda mpaka kufika 2025 mimi nina uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema tuendelee na CCM,tuendelee na Rais Samia Suluhu Hassan. Hatutokuwa na sababu nyingine yoyote kwanza ni utamaduni wetu Chama Cha Mapinduzi hatubadilishi uongozi katikati ya safari,ukitaka kubadilisha sababu itakuwa nini, hakuna.

“Lazima tumpe mtu nafasi yale aliyokusudia chini ya uongozi wa Chama chetu yatimie, ikifika 2025 tunakwenda na Rais Samia na Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa amesema kila eneo,kila kata,kila mtaa kila jimbo yako ya kusemea mema,hatuahidi miujiza lakini tumeahidi na yale tuliyoahidi tumeyatekeleza kwa ufanisi mkubwa sana.

“Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM lakini tunaangalia na wenzetu wa nchi jirani wanakwendaje. Nchi yetu imetulia,inamaani,ina umoja,inamshikamano, nchi ina malengo, na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina Ilani nzuri inayotekelezeka,” alisema Kinana.

Aidha,alisema kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya udini wameshindwa, kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ukabila wameshindwa, kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ubara na visiwani wameshindwa huku akifafanua katika Bara la Afrika ziko nchi nyingi zimeajaribu kuungana na wanazifahamu ikiwemo Afrika Magharibi na nchi za Uarabuni zote zimesambaratika umoja haupo,lakini Tanzania muungano wao umeendelea kuwa imara na mwakani muungano huo unafikisha miaka 60.

“Sababu ni misingi imara iliyojengwa na wasisi wa taifa letu hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Abeid Aman Karume,misingi yenyewe migumu na mnakumbuka katika kipindi mbalimbali muungano wetu umepitia kashikashi lakini tumeendelea kuwa imara,” alisema.

Pamoja na hayo Kinana alisema anaungana na wananchi wote pamoja na viongozi kumpongeza Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia kwa uongozi wake madhubuti. “Wakati mwingine baadhi ya watu wanaona kama vile labda tunamsifu sana ndugu Rais lakini hatumsifu kwa mambo ambayo hayana uhakika,kama nilivyosema ushahidi upo.”

“Baadhi yenu mlifuatilia Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma mwezi wa 12 taarifa ilitolewa pale ikaelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya miaka miwili na miaka miwili hiyo wakati huo ilikuwa ni ya Rais Samia. Amefanya kazi kubwa sana na ili muweze kutekeleza kazi zenu vizuri lazima muwe na fedha za kutosha.

“Fedha hizo ni mapato ya ndani,mapato ya nje. Mapato ya ndani ya makusanyo yaliyokusanywa na serikali na taasisi zake mbalimbali miaka hii miwili kwa kila mwezi yako juu kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu,makusanyo yamefanikiwa bila mtu kusukumwa,bila kutishwa bila mtu kuwekwa mahabusu.

“Mapato kutoka nje yamekuja kwa sababu Rais na serikali yake chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi wamejenga mahusiano mazuri sana,dunia leo inatuamini zaidi,inatuheshimu zaidi,inatuthamini zaidi,nchi inakopesheka kuliko wakati wowote. Hivi karibuni kulikuwa na mashirika mawili duniani ambayo yanafanya tathimini ya hali ya uchumi na namna nchi inavyoweza kukopesheka.

“Mashirika yote mawili yametoa alama ya juu sana kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,maana yake ni nini ukitaka kupewa msaada hawa wanaaminika, watatumia misaada vizuri hawataiba,hawatatumia vibaya,hatawapoteza mkitaka kwenda kutafuta mkopo kwa tathimini yao Tanzania tunakopesheka,”alisema.

Awali akielezea utekelezaji wa Ilani katika Jimbo la Kondoa Vijijini Dk.Kijaji alimpongeza Rais Samia kwa kuitazama kwa karibu Kondoa ambapo katika kipindi cha miaka miwili na nusu miradi ya maendeleo imepelekwa katika sekta mbalimbali na hiyo ni kutekeleza ahadi ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi.

“Kwa kipekee nimshukuru Serikali ya CCM ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Dk.Samia kwa kutekeleza kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

Kwa wananchi wetu wa Jimbo la Kondoa kila mmoja wetu anaona kwa macho miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika vijiji na vitongoji,hivyo basi naomba muendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi.”

Wakati wabunge na Wajumbe wa Halmashauri ya Taifa(NEC)ambao wamepata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo wameeleza kwa kina hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya bandari nchini huku wakitoa rai kwa wananchi kutosikiliza maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya watu ambao kimsingi wameishiwa hoja.

Oliver G Nyeriga - MTV TANZANIA