Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania kupitia Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini (REGROW) inatarajia kujenga kituo kikubwa cha kutoa taarifa za utalii Kusini katika eneo la Kihesa Kilolo Mkoani Iringa kwa fedha zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa lengo la kukuza utalii wa ukanda huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Mhe.Angellah Kairuki ameyasema hayo katika ufunguzi wa Maonesho ya "Utalii Karibu Kusini" yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Kihesa Kilolo Mkoani Iringa.
Sambamba na kituo hicho, Mhe. Kairuki ameitaja Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori –(MWEKA)
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha - AICC pamoja Chuo cha Taifa cha Utalii ( NCT) zitaanzisha matawi yao ili kulifanya eneo hilo la Kihesa Kilolo kuwa eneo mahiri kwa Utalii Kusini.
Amesema hizo zote ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuendeleza na kukuza Sekta ya Utalii nchini hususani Kusini.
Aidha, amesema kufanyika kwa Maonesho hayo kutasaidia kukuza Sekta ya Utalii Kusini ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya ‘The Royal Tour’ ambapo idadi ya watalii imekuwa ikiendelea kuongezeka kwa kasi.
Katika hatua nyingine, ili kuendelea kukuza utalii Kusini, Mhe. Kairuki ameweka bayana kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ikiwemo kujenga Uwanja wa Ndege wa Songwe Jijini Mbeya; kupanua uwanja wa ndege wa Iringa kwa zaidi ya shilingi bilioni 66; kujenga na kupanua barabara za katikati ya miji mfano Ujenzi wa barabara ya njia nne katika jiji la Mbeya yenye urefu wa kilomita 29 kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 138.7.
Pia, amesema Serikali imesaini Mkataba wa zaidi ya Shilingi trilioni moja (1) kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Igawa – Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 na imeendelea kujenga barabara zinazoelekea katika vivutio vya Utalii akitolea mfano wa ujenzi wa barabara ya Njombe - Makete yenye urefu wa kilomita 109 itakayosaidia watalii kufika kirahisi katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
Sanjari na hayo, Mhe.Kairuki amesema Serikali imefanya ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 16 inayoelekea kwenye Maporomoko ya Kalambo pia imejenga ngazi kushuka chini kuelekea katika maporomoko hayo na imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Iringa kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa ukubwa kilomita 104.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Halima Dendego amesema kupitia Maonesho hayo wawekezaji na idadi ya watalii imeongezeka hivyo kusaidia kukuza utalii Kusini.
Maonesho hayo yenye kaulimbiu "Utalii Karibu Kusini mwelekeo mpya wa uwekezaji" yanayofanyika kwa muda wa siku tano (5) yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo Kongamano la Uwekezaji, Mbio za Marathoni, Mbio za magari, kutembelea vivutio vya utalii katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa na kushiriki katika shughuli za kitamaduni.