Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.
Pia, Mhe. Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi waimarishe huduma za uwezeshaji ili waweze kuyafikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati akifunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. “Suala la kuanzisha vituo vya uwezeshaji ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 katika Ibara ya 26 (k) na hili ni jukumu letu viongozi kuhakiksha ilani inatekelezwa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe wanaimarisha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ambazo zitawaongezea kipato.
“Katika hili ninawapongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuwezesha Jukwaa la Mkoa kuanzisha SACCOs 76 za wanawake zenye wanachama 322 pamoja na Halmashauri ya Ushetu ambayo imeanzisha Jukwaa linaloendesha Mradi wa Kampuni ya Usafi wa Mazingira na usindikaji wa mboga za majani maarufu kwa jina la Nsansa.”
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa alisema kongamano hilo linalenga kuongeza ufahamu wa wadau mbalimbali kuhusu dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuwakumbusha majukumu waliyonayo katika kuwawezesha Watanzania.
Alisema malengo mengine ni pamoja na wadau kupeana uzoefu katika kutekeleza shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuzindua taarifa ya mwaka 2022/2023 ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo pia imejumuisha masuala ya ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.
Katibu Mtendaji huyo alitaja kaulimbiu ya kongamano hilo kuwa ni “Uwezeshaji kwa Uchumi Endelevu”. “Kaulimbiu hii inaendana na azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watanzania wanawezeshwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi ili kuweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.”
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023, mifuko na programu za uwezeshaji ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 743.7 kwa wanufaika wapatao 6,064,957 ambapo miongoni mwao wanaume ni asilimia 46 na wanawake asilimia 54.