Wanawake nchini Tanzania wametakiwa kuungana na kushikamana imara zaidi ili kufikia malengo ya ajenda ya maendeleo ya wanawake hasa usawa wa kijinsia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Kongamano la miaka 25 la Chama cha Wanawake Wachimba Madini (TAWOMA) lililofanyika mkoani Geita.
Waziri Gwajima amewataka kutambua umuhimu wa kushikamana na kushirikiana, kuepuka kukatiliana bali kusaidiana katika kila hali ambapo amewahakikishia TAWOMA na wanawake kwa ujumla kuhusu dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwainua wanawake ambayo ameianza tangu akiwa Makamu wa Rais.
"Ndiyo maana mara tu alipoapishwa kuwa Rais aliamua kuunda Wizara mahsusi ya kushughulikia masuala ya wanawake. Hivyo natoa wito kwa wanawake kutambua na kuthamini dhamira hii kwani siyo rahisi kupata kiongozi anayedhamiria kuleta mabadiliko ya maendeleo kwa jicho la usawa wa kijinsia.
“Wanawake mmepata mtetezi makini wa ajenda za wanawake hivyo msipomshikilia mtazunguka sana miaka mingi kufikia malengo ya usawa wa kijinsia, mshikilieni awavushe” Waziri Dkt. Gwajima.
Wakati huo huo, Dkt. Gwajima ameelekeza Uongozi wa TAWOMA kukusanya changamoto za wajasiriamali wa madini nchi nzima na kuwasilisha kabla ya Novemba, 2023 ili zitafutiwe majibu na kuandaa tamasha kubwa la wanawake sekta ya madini Januari 2024.
Ametumia nafasi hiyo pia kusikiliza hoja za wanawake wachimba madini ambapo, changamoto kubwa zilizoibuliwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji, vifaa vya kazi, maeneo ya kuchimba madini, changamoto za leseni na mafunzo kuhusu ujasiriamali husika. Aidha, pamoja na changamoto hizo, amewapongeza kwa kufanikiwa kuhamasisha wanawake wengi kujiajiri kupitia sekta ya madini na kuwaweka pamoja.
Hali kadhalika, Dkt. Gwajima, ametambua mafanikio ya kihistoria ya Mjasiriamali Sarah Masasi ambaye amefikia hatua ya kumiliki kampuni na kiwanda cha kusafisha dhahabu yote inayotoka mkoa wa Geita inayopelekwa BOT na nje ya nchi, ambapo, amemteua kuwa Mwenyekiti mwenza kwenye maandalizi ya tamasha hilo ambapo ni moja ya ombi la wanachama wa TAWOMA.
Naye Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza katika kongamano hilo, amesema Wizara ya Madini kupitia Shirika la Taifa la Madini STAMICO, imeendelea kuimarisha ufanisi wa wachimbaji wanawake ikiwemo kufanya utafiti kwenye mikoa minne kujua changamoto za wachimbaji wanawake, kutafuta vifaa na kuwapa mafunzo.
"Tayari maeneo 15 yamepatikana kwa ajili ya wachimbaji wanawake katika mkoa wa Geita, habari njema ni kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye amesema atalipia leseni zote za maeneo hayo" amesema Mhe. Mavunde.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa Semeni Malale amemshukuru Rais Samia kwa kuwajali wanawake wachumbaji kwani wanafanya kazi kwa weledi tofauti na awali ambapo walikuwa wanasemwa wana mkosi kufanya kazi migodini.