TANZANIA

Wananchi Watakiwa Kutoa Ushirikiano kwa Tafiti Zinazofanyika Nchini

JANUARI 15, 2024
Border
news image

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania Mhe. Rosemary Senyamule amefanya Mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia utafiti wa shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanyika katika mikoa yote ukiwemo Mkoa wa Dodoma kwenye ukumbi wa ofisi yake Jijini Dodoma.

Utafiti wa kilimo unaofanyika ni wa mwaka wa kilimo 2022/23 ambapo tafiti hizi zinaiwezesha nchi yetu kupata Takwimu Rasmi ambazo zinatumika katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo za kikanda na Kimataifa.

"Utafiti huu utafanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kwa kipindi cha siku 60 na umeanza Tarehe 5 Novemba 2023. Utafiti huu ni muhimu sana kwa kuwa sekta ya kilimo inachangia wastani wa asilimia 26.2 ya pato la Taifa, inatoa ajira kwa karibu asilimia 65 ya watu wote nchini, inatuhakikishia usalama wa chakula na ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta nyingine hususani viwanda.

"Utafiti wa kilimo mwaka 2023/24 utafanyika Tanzania nzima kwenye jumla ya maeneo 1,352. Kati ya maeneo hayo , 1,234 ni ya Tanzania Bara na maeneo 118 ni Zanzibar. Jumla ya kaya za Kilimo 16,224 zitahojiwa nchi nzima. Kati ya hizi 14,808 ni za Tanzania Bara na 1,416 ni za Zanzibar. Utafiti huu utafanyika katika ngazi ya Kaya na katika ngazi ya Taasisi. Katika Mkoa wetu maeneo yaliyochaguliwa kufanyika utafiti huu ni 61" Amesema Mhe. Senyamule

Aidha, Mhe. Senyamule ametoa shime kwa wananchi kutoa ushirikiano pindi wanapohitajika kufanya hivyo kwani kadri wanaposhiriki katika tafiti hizi ndivyo Serikali inapogundua changamoto zinawakabili na hatimaye kuchukua hatua stahiki. Pia amesema kushiriki tafiti ni sehemu ya mchango katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu na maendeleo ya nchi nzima.

Tafiti hizi zinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura 351 ambayo inaipa mamlaka ya Kisheria ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufanya tafiti mbalimbali za Kitakwimu ili kuzalisha Takwimu kwa ajili ya kutumika katika kutunga na kuhuisha sera, kupanga mipango na programu za maendeleo na kufuatilia na kutathmini utekelezaji wake.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania