TANZANIA

Wananchi Tanzania Watakiwa Kuomba Kibali Kutumia Sare za Jeshi

AGOSTI 24, 2023
Border
news image

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa Siku saba (7) kwa wafanyabiashara wanaongiza nchini mavazi yenye mfanano na sare za Jeshi hilo na kuja kuyauza kwa baadhi ya raia kupitia maduka au maeneo yao ya biashara kuyasalimisha ndani ya siku saba kabla hatua zaidi hazijaanza kuchukuliwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi hilo Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma na kusema wapo baadhi ya raia na wengine ni wasanii wanaovaa mavazi hayo ya jeshi na kuyatumia kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu hivyo kwanzia sasa wanapaswa kuwa na kibali iwapo wanahitaji kuyatumia mavazi hayo.

''Wapo baadhi ya wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu hivyo kwanzia sasa wanapaswa kuwa na kibali iwapo wanahitaji kuyatumia mavazi hayo''amesema Luteni Kanali Ilonda.

Aidha amesema katazo hilo ni kwa Mujibu wa Kifungu cha 99 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa sura ya 192 sheria namba 24 ya mwaka 1966 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

''Aidha,kifungu cha 178 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16(Penal Code) na kifungu cha 6 cha Sheria ya Usalama wa Taifa vinakataza Raia kuvaa sare na mavazi ya Majeshi ya Ulinzi au yanayofanana nayo''amesema.

Amehitimisha kwakusema vitendo vya uvunjifu wa sheria za nchi kama hivyo havipaswi kufumbiwa macho na endapo hali hiyo ikiachwa iendelee inaweza kuhatarisha Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania