Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)Dkt. Selemani Jafo amewahimiza wananchi kulinda mazingira kwani yakiharibika uchumi utayumba.
Ametoa kauli hiyo alipotembelea Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya EPZ Bombambili mkoani Geita.
Akizungumza wakati akitembelea Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alisema bila kutunza mazingira fedha hazitapatikana kwa kuwa shughuli za maendeleo zikiwemo kilimo, uvuvi na mifugo zitayumba.
Dkt. Jafo amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi husababisha ukame ambao huathiri kilimo na mifugo kukosa maji na kufa hali inayosababisha mzunguko wa fedha kuwa mdogo.
“Leo hii kukitokea ukame mifugo itakufa na wakulima watashindwa kulima na yote haya ni mabadiliko ya tabianchi hivyo nawaomba wananchi wapande miti na kutunza mazingra kwa ujumla,” amesema Dkt. Jafo.
Hali kadhalika ametoa rai kwa BoT na kuibenba Sera ya Mazingira kwani ndio ni mojawapo ya injini ya uchumi kwani mazingira yakiharibika na uchumi unadorora.
Ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi kuipitia sekta ya madini na kuimarisha miundombinu.
Aidha, amewapongeza BoT kwa kusimamia vyema fedha pamoja na kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni hivi karibuni lakini wameonesha uimara.
Pia, Waziri Dk. Jafo ameitaka taasisi hiyo kusimamia matumizi ya fedha mtandao ili kuwapisha wananchi kutembelea na maburungutu ya fedha hali ambayo si salama.