KENYA

Wanajeshi Wa Kenya Wajeruhiwa Kwenye Shambulizi La Kilipuzi

SEPTEMBA 11, 2023
Border
news image

Kikosi cha ulinzi nchini Kenya KDF- kimethibitisha kuwa baadhi ya wanajeshi walijeruhiwa jana baada ya lori lao kukanyaga kilipuzi huko Baure, Kaunti ya Lamu. Kwenye taarifa, KDF ilisema lori la kikosi hicho lilikuwa likiwasafirisha maafisa wake kwenye barabara ya kutoka Baure kuelekea Drum wakati lilipokanyanga kilipuzi hicho.

Shambulizi hilo liliwajeruhi wafanyikazi na kuharibu karadinga la Jeshi la Kenya. KDF ilisema waliojeruhiwa walikimbizwa katika kituo cha Manda kwa matibabu. Ikishtumu kisa hicho, KDF ilitoa wito kwa wenyeji kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu wahalifu wanaojificha katika jamii.

Hili ni tukio la hivi punde zaidi mwezi huu. Mwezi Agosti, zaidi ya watu 10 waliuawa katika eneo hilo katika mashambulizi tofauti yanayohusiana na ugaidi.

AM/MTV NEWS