TANZANIA

Wachimbaji Wadogo Wa Madini Tanzania Watakiwa Kuchangamkia Fursa Za Utafiti

SEPTEMBA 22, 2023
Border
news image

Wachimbaji wa Madini nchini Tanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za taarifa za utafiti wa Madini zinazofanywa na Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuchimba kwa tija.

Hayo yamebainishwa leo na Mjiolojia Mwandamizi Deogratius Oreku wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alipotembelea Banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake katika maonesho ya sita (6) ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Mapema baada ya kupata taarifa za maendeleo ya Sekta ya Madini , Naibu Waziri alitaka kufahamu kuhusu taarifa za utafiti ili kuwasaidia wachimbaji wadogo katika uchimbaji Madini.

Akifafanua kuhusu taarifa za utafiti zinazotolewa na Wizara kupitia machapisho mbalimbali , Oreku amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia kitabu cha Mwongozo wa Wachimbaji Madini Wadogo kimekuwa msaada mkubwa kutokana na taarifa zilizochapishwa kuhusu hatua za utafutaji Madini.

Sambamba, na mwongozo huo Wizara kupitia Taasisi zake imefanya utafiti wa kina katika maeneo saba yaliyotengwa kwa ajili ya uchimbaji mdogo ambapo utafiti wa awali wa jiolojia umefanyika kwa asilimia 97, Jiokemia asilimia 23 na Jiofizikia asilimia 16 hivyo wachimbaji wadogo wanaweza kutumia taarifa hizo ili waweze kuchimba kwa urahisi na uhakika.

Maonesho ya sita ya Tekinolojia ya Madini kwa mwaka 2023 yanaongozwa na kaulimbiu inayosema " *Matumizi Sahihi ya Teknolojia katika kuinua wachimbaji wadogo kiuchumi na kuhifadhi mazingira"

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania