TANZANIA

Utekelezaji wa Miradi ya Elimu Iendane na Mazingira Salama kwa Wanafunzi Tanzania

SEPTEMBA 21, 2023
Border
news image

Wataalam kutoka Benki ya Dunia wamewashauri wasimamizi wa elimu nchini Tanzania kuzingatia usalama wa watoto ndani na nje ya shule kwa kuimarisha usimamizi wa mazingira katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.

Hayo yamebainishwa na Mtaalam anayeshughulikia Masuala ya Jamii na Usalama kutoka Benki ya Dunia Dkt.Naima Besta kwenye ziara ya kikazi iliyowashirikisha timu ya Wataalam OR- TAMISEMI, Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia na Wadau wa Benki ya Dunia lengo likiwa ni kukagua utekelezaji wa miradi ya elimu SEQUIP na BOOST Mkoani Kigoma.

Amewaelekeza wasimamizi wa elimu nchini kuzingatia usalama wa watoto na mazingira kwa kuwapa nafasi ya kujadili changamoto zao kwenye mabaraza ya wanafunzi, kuwepo na walimu wa nasihi ambao watasikiliza na kushughulikia maoni yao.

"Usalama wa mtoto ni pamoja na shule hizo kuweka vibao vya matangazo ili kuonesha ujumbe kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla" amesisitiza

Naye, Mratibu wa Shule Salama Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bi. Hilda Mgomapayo amesema, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kwa kuweka mazingira salama kwa watoto kuanzia Elimu ya Awali, Msingi hadi Sekondari kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kukamilisha mzunguko wao wa elimu.

Amesema mazingira salama ya mtoto ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wanafunzi, kuimarisha, mahusiano na ushirikiano kati ya shule na jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kudhibiti hali ya utoro na kuimarisha huduma ya chakula shuleni.

"Tuendelee kutoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia,mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili ukiwa ni pamoja na kuweka masanduku ya maoni,vibao vinanavyotoa elimu mbalimbali ikiwemo VVU/UKIMWI, ukatili na usawa wa kijinsia bila kusahau huduma ya kwanza mahala pa ujenzi" amesisitiza

Awali akisoma taarifa ya ujenzi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bondo Oscar John amesema, shule hiyo imepokea Tsh. mil. 110 kupitia Mradi wa BOOST kujenga madarasa 4 na matundu ya vyoo 3 ambapo ujenzi umekamilika

Ameeleza katika ujenzi huo wamezingatia kuweka alama zote za kuonesha usalama na mazigira ya mtoto kwa kuweka vibao vya matangazo ili kutoa elimu kupitia hasa usalama wa mtoto na mazingira ili watoto hao waweze kutimiza malengo yao.

Mwl. John ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa shule hiyo sababu imesaidia kupunguza changamoto ya elimu katika Kijiji cha Kasuku Kata ya Simbo.

Timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia wapo kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa BOOST na SEQUIP.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania