TANZANIA

Tunafanya Kila Jitihada Kupunguza Makali Ya Umeme Nchini-Dkt. Doto Biteko

OKTOBA 03, 2023
Border
news image

Naibu Waziri Mkuu nchini Tanzania na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Wizara ya Nishati inafanya jitihada mbalimbali ili kupunguza makali ya umeme nchini na hivyo kuwaondolea wananchi matatizo ya umeme wanayoyapata kwa sasa.

Amesema hayo baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Nyanguku na Bunegezi wilayani Geita, Mkoa wa Geita ambapo pia alizungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara katika vijiji hivyo.

“Tumekubaliana, Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi warudi Dodoma kushughulikia masuala ya mgawo wa umeme, tunataka tupunguze mgao huu kwa kasi kubwa ili wananchi wasipate matatizo ya umeme, vilevile Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga anatembelea vituo vya kufua umeme, alianzia Ubungo, ameenda Tegeta na maeneo mengine, lengo letu ni lile, kupunguza makali ya mgawo wa umeme kwa watu wetu.”Amesema Dkt. Doto Biteko

Ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati inalitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kushughulikia changamoto za upatikanaji umeme wa uhakika ndani ya miezi sita ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila matatizo.

Kuhusu umeme vijijini amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inataka umeme uwafikie wananchi wote na kwa Mkoa wa Geita imetoa shilingi bilioni 39 kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini mkoani humo na dhamira ya Serikali ni kufikisha umeme kaya kwa kaya.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza suala la viongozi kusimamia fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, wawahudumie wananchi na kuwapa nyenzo za kuwawezesha kufanya kazi ili wajikwamue katika maisha yao.

“Tunachotaka ni kuona kila senti iliyokusudiwa kwa ajili ya miradi inawafikia wananchi, umetaka iwafikie, hutaki mwachie mwingine anayetaka kuwahudumia wananchi, na nyie wananchi miradi ikijengwa kwenye eneo lenu msiiache bali nendeni mkaisimamie kwani tunachotaka kuona hii miradi inamilikiwa na wananchi.”amesisitiza Dkt. Biteko

Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, alisema kuwa, Mkoa wa Geita una 486 na hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, REA imeshapeleka umeme kwenye vijiji 359 na vijiji vilivyobaki tayari mkandarasi anaendelea na kazi na ameshaanza kuwasha umeme kwenye vijiji alivyokabidhiwa.

Ameongeza kuwa, kwa Wilaya ya Geita Serikali imetoa shilingi Bilioni 2 ili kupeleka umeme kwa vijiji vilivyopo wilayani humo na shilingi bilioni 6.9 zimetolewa kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vijiji-miji vya wilaya ya Geita.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania