TANZANIA

Ujenzi wa Miradi Minne ya Umwagiliaji Wilayani Mbulu Kuanza Rasmi

SEPTEMBA 28, 2023
Border
news image

Ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kufanya mageuzi kabambe ya Kilimo Nchini, Tume ya Umwagiliaji imetoa taarifa rasmi ya kuanza upembuzi yakinifu wa miradi mikubwa ya Umwagiliaji itakayo tekelezwa Wilayani Mbulu.

Wakizungumza mapema katika zoezi la kuwatambulisha Wataalamu na kampuni zilizokabidhiwa jukumu hilo, kwa Mkuu wa wilaya ya Mbulu Komred Kheri James. Wameeleza kuwa zoezi la upembuzi yakinifu litafanyika kwa muda wa miezi sita, na maeneo yatakayo jengewa miradi hiyo ni Tumati, Dongobesh na Dirim.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu Komred Kheri James, Amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huo muhimu utakao ongeza tija kwa wakulima na kilimo kwa ujumla, na amewataka viongozi na Wananchi katika maeneo tajwa watoe ushirikiano katika hatua zote za zoezi hilo muhimu ili kurahisisha na kuharikisha utekelezaji wa ratiba ya mradi.

Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa wilaya ambazo asilimia kubwa ya Wananchi wake wanaishi kwa kutegemea kilimo, hivyo ujio wa miradi hii ni chachu ya kiuchumi na kijamii kwa Wananchi.

Zoezi la upembuzi yakinifu kwa wilaya ya Mbulu,litafanywa na kampuni tatu ambazo ni CCL, Mult-Tech Consult na Netwas Tanzania Ltd.Kampuni zote zitafanya wajibu wake chini ya usimamizi wa Tume ya Umwagiliaji.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania