TANZANIA

Ubunifu Suluhu Ya Mapato Vyuo Vyamaendeleo Ya Jamii Tanzania - Dkt. Gwajima

AGOSTI 24, 2023
Border
news image

Serikali ya Tanzania imesema ubunifu wa miradi utasaidia vyuo vya Maendeleo ya Jamii kukusanya mapato zaidi na kujiendesha kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima alipokua akijibu hoja mbele ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao na Kamati hiyo juu ya uendeshwaji wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Rugemba Jijini Dodoma.

Waziri Dkt. Gwajima amesema endapo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vitaweza kuwekeza katika ubunifu wa miradi mbalimbali itakuwa ni njia ya haraka ya wao kupata pesa ambazo zitawawezesha kujiendesha na kupunguza utegemezi Serikali kuu.

“Tukiwekeza kwenye miradi yetu kama kilimo,ufugaji na miradi mingine mingi kulingana na eneo husika kwa ubunifu na ustadi naamini tutaweza kuongeza kipato na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini “alisema Dkt. Gwajima.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema suala la uanagenzi ni jambo linalofanyika katika Vyuo vyote vya Maendeleo ya jamii nchini ili kutoa wataalam wenye ujuzi watakaweza kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Jamii na Taifa.

“Mbinu ya Uanagenzi inatumika katika vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ikiwa na dhumuni la kuwanoa wanafunzi katika maeneo muhimu waliojifunza Vyuoni kwani mafunzo hayo ni zaidi ya mafunzo kwa vitendo maana wanafunzi hupata muda zaidi wa kuweza kuimarika katika eneo husika.” alisema Dkt. jingu

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq, ameishauri Serikali kushirikiana na wadau tofauti wa maendeleo kwenye kukuza miradi iliyopo katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili iweze kusaidia katika uendeshaji wa Vyuo hivyo.

“Ili miradi hii ikue ni vyema mkitumia mbinu ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo waasisi wa chuo hiki waliokuwa na lengo la kusaidia watoto wa kike. Njia hii inaweza kuchochea mafanikio makubwa na yenye uendelevu” alisema Toufiq

Sambamba na hilo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipitishwa kwenye wasilisho la mfumo wa Kidigitali wa taarifa wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ambao umetengenezwa ili kuleta uwazi na uwajibikaji kwa wadau wote wa NGOs nchini.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania