TANZANIA

Tuongeze Nguvu Zaidi Kupambana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu Ili Tuutokomeze Ifikapo 2030

SEPTEMBA 23, 2023
Border
news image

Waziri wa Afya nchini Tanzania Mhe.Ummy Mwalimu ametoa rai kwa Jumuiya za Kimataifa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa kuongeza nguvu zaidi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuweza kuutokomeza kabla ya Mwaka 2030.

Waziri Ummy amesema hayo alipokuwa akitoa tamko la Tanzania kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwenye vikao vinavyoendelea vya Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa.

“Bado hakuna rasilimali za kutosha kupambana na TB, tunaendelea kuhimiza wadau wa Sekta ya Afya kuunganisha nguvu za pamoja na kuwekeza zaidi kwenye rasilimali, tafiti, teknolojia, vifaa na vifaatiba” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye watu wengi wenye maambukizi ya Kifua Kikuu ikichangia asilimia 87 ya ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani.

“Takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu 132,000 wanaogua ugonjwa wa kifua Kikuu, tumeweza kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huu kwa asilimia 32 na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 55” amesema Waziri Ummy na kusema kuwa Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuutokomeza ifikapo 2030.

Katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomea ifikapo mwaka 2030, Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imewekeza nguvu kubwa kwenye utoaji wa matibabu ya Kifua Kikuu pamoja na utoaji wa elimu ya afya ili jamii iweze kufahamu ugonjwa huo mapema na kupata matibabu.

Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati Shirikishi wa Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu uliozinduliwa mwezi machi 2023 utakaosaidia kuongoza katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.

Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania inaungana na nchi nyinginezo chini ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa huo na imeridhia azimio lililowekwa la kuendelea na mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania