Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini Tanzania (TMDA) Kanda ya Mashariki imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya utupaji holela wa dawa zinazobaki majumbani kutokana na hatari zake kwa afya ya binadamu na mazingira.
Akizungumza wakati wa zoezi la kutoa elimu katika shule ya Sekondari ya wasichana Bibi Titi Mohamed iliyopo Halmashauri ya Rufiji Mkoa wa Pwani, Mkaguzi wa Dawa Kanda ya Mashariki Bw Japhari Saidi ameeleza kuwa dawa zinazobaki majumbani hazipaswi kutupwa jalalani, chooni, kwenye vyombo vya kukusanya taka au kuchomwa moto katika maeneo ya wazi badala yake zirudishwe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali au ofisi za TMDA zilizopo jirani.
Akifafanua athari za kutupa dawa kiholela Bw Japhari amesema " Dawa zinapotupwa jalalalani au kwenye vyombo vya kukusanya taka, watu wasio waaminifu wanaweza kuziokota, wakazisafisha na kuziweka lebo za kughushi na kisha kuzirudisha mtaani ziendelee kutumika hata baada ya kwisha muda wake wa matumizi.
"Vile vile, kwa kuwa dawa ni kemikali zinapotupwa kiholela zinabebwa na maji na kupelekwa kwenye vyanzo vya maji na hivyo kuchafua maji na wanyama wa majini wanaoliwa na binadamu kitu kinachoweza kusababisha magonjwa mbalimbali.
Akifafanua zaidi Bw Japhari amesema, dawa zilizokwisha muda wa matumizi zinapochomwa kwenye eneo la wazi huzalisha kemikali mbalimbali zinazochafua hewa na hivyo binadamu wanaovuta hewa hiyo wanaweza kuathirika ikiwemo kupata matatizo ya kupumua, saratani ya mapafu, mzio na mengine
Japhari ameeleza kuwa hata ukitupa dawa kwenye shimo la choo bado kemikali zilizomo zinaweza kuuwa vijidudu vinavyosaidia kinyesi kuoza vizuri na hivyo kusababisha vyoo kutoa harufu kali.
Amewataka wananchi kuacha kufanya hivyo badala yake wazikusanye dawa zilizobaki majumbani kwa sababu yeyote ile na kisha wazipeleke kwenye vituo vya afya vya serikali au ofisi za TMDA zilizopo karibu ili ziharibiwe kwa njia zilizo salama kwa binaadamu na mazingira.
Akihitimisha zoezi la uelimishaji kwa Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani lililofikia shule 13 za sekondari, Bw Japhari ametoa wito kwa wanafunzi na waalimu waliopata elimu hiyo kuendelea kuisambaza kwa jamii ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.