Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza wataalamu wa mifumo na TEHAMA, wabuni programu tumizi ya kuweza kutambua risiti halali na zisizo halali ili kujihakikishia kuwa mapato yote yanayokusanywa yanaingia Serikalini.
Kadhalika, amewataka waweke utaratibu wa kufanya kaguzi za mashine za “PoS” ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote unaofanyika sambamba na kuwa na utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na mfumo wa usalama maalum wa utunzaji taarifa (back-up).
Ameyasema hayo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma.
“Niwakumbushe watumishi wa umma kuwa bado tunalo jukumu la kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyosisitiza juu ya usimamizi wa ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa mjini Kibaha.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali iliunda mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama TAUSI ili kupunguza urasimu uliokuwepo kwenye ukusanyaji wa mapato. “Mfumo huu mpya ni wa kidijitali na humrahisishia mfanyabiashara kufanya malipo ya Halmashauri kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu yake ya kiganjani au kompyuta”
“Mfumo huu umelenga kumsaidia mteja kujihudumia mwenyewe, hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba au kulipia tozo, ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali. Badala yake anaweza kufanya mwenyewe kupitia dirisha la mteja au Taxpayer Portal.”
“Nipende kuwasisitiza wafanyabiashara na watoa huduma watoe risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja. Kwa upande wa wateja, niwakumbushe kuwa ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa, amewataka waajiri wachukue hatua za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi vilivyomo katika maeneo yao ya kazi.
Hatua hizo ni pamoja na kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi, kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya ili kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi na kulinda uwekezaji wao.
“Nitoe wito kwa watumishi wa OSHA wawe waadilifu wanapoendesha mazoezi ya ukaguzi mahali pa kazi na kuchukua vipimo vya wafanyakazi.”
Pia amewataka, Wafanyakazi wahakikishe wanazingatia taratibu na miongozo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza watendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo. Vilevile, waajiri watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa wakati michango katika mfuko huo.