TANZANIA

Temesa Mpya Inayotoa Huduma Bora Inakuja: Bashungwa

OKTOBA 04, 2023
Border
news image

Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania Mhe.Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inakwenda kufanya maboresho makubwa ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ili kuhakikisha wanatoa huduma bora na ya kuridhisha kwa wadau wake ambao wamekuwa  wakilalamikia taasisi hiyo.

Ameyazungumza hayo mkoani Mbeya nchini Tanzania wakati Waziri huyo alipokagua karakana ya TEMESA ambayo ni kati ya karakana 26 zinazosimamiwa na Wakala huo na kutoa wito kwa wadau kuendelea kuwa na imani na Taasisi hiyo kwani Serikali inaendelea kuifanyia maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inapatiwa fedha za kununua vifaa na kuboresha rasilimali watu.

“Ninatambua kuna malalamiko mbalimbali kuhusu masuala ya vipuri feki na TEMESA kutokuwa na uwezo wa kutengeneza magari na badala yake kupeleka kwenye garage nyingine ya mtaani lakini sasa niwahakikishie kuwa tunaenda kuibadilisha TEMESA ili kila mteja atamani kuleta gari lake hapa”, ameeleza Bashungwa

Bashungwa ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kutoa fedha za kuiwezesha TEMESA inapata vifaa vya uhakika vya kutengeneza magari pamoja na watumishi wa kutosha.

Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mtendaji Mkuu TEMESA kukaa na kampuni ya TOYOTA na kuweka mikakati namna ambavyo wanaweza kushirikiana kwa ubia ili kampuni hiyo iweze kuhudumia karakana zote nchini.

“Ninaamini ushirikiano wa kimkakati kati ya TEMESA na TOYOTA unaweza kuwa ni mwarobaini wa changamoto ambazo wadau mbalimbali wamekuwa wakiilalamikia TEMESA”, amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amewataka Mameneja wa mikoa kubainisha kesi zozote zinazotokana na watumishi wasio waaminifu katika matengenezo ya magari kwa kuchukua hatua kali bila kupepesa macho.

“Mameneja wote wa mikoa ya TEMESA timizeni wajibu wenu kama inavyostahili na kuchukua hatua pale mnapobainisha wezi msipofanya hivyo Serikali itawashughulikia ninyi”, ameongeza Bashungwa.

Bashungwa amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa TEMESA pamoja na Mameneja wake kutoka mikoa yote watumie mikakati bora ya utoaji huduma kwa wateja ili kuweza kufanya biashara na kuingizia Wakala huo mapato.

Kuhusu suala la madeni ya Wakala huo, Bashungwa amezitaka Taasisi zote za Serikali, Wadau mbalimbali wanaopata huduma kwa Wakala huo kulipa madeni hayo kwa wakati ili kuiwezesha TEMESA kuendana mabadiliko chanya yanayotarajiwa kufanyika.

Naye, Meneja wa TEMESA mkoani Mbeya Eng. Clement Abadyame ameahidi kuendelea kutoa huduma kwa wateja na kuimarisha utoaji huduma ili wateja waweze kupata huduma bora kulingana na thamani ya fedha kwani fedha inayotumika kutengeneza magari hayo ni ya watanzania.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania