UFARANSA

Tanzania Yatangaza Utajiri wa Madini Mkakati Ufaransa

SEPTEMBA 29, 2023
Border
news image

Naibu Waziri wa Madini kutoka nchini Tanzania Dkt.Steven Kiruswa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye rasilimali madini kwa wingi yakiwemo Madini Mkakati ambayo mahitaji yake yanazidi kuongezeka kutokana na kutumika kuzalisha aina tofauti za vyanzo vya nishati na teknolojia zinazohitaji aina mbalimbali za madini mkakati kama vile Lithiamu, Nikeli, Kobalti, Manganese na Grafiti.

Ameyasema hayo jijini Paris nchini Ufaransa wakati akihutubia Mkutano wa Kilele wa Usalama wa Madini Mkakati ambao umejadili masuala muhimu kuhusu madini hayo, kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili namna ya kushiriki katika kuchochea usimamizi na usambazaji endelevu wa madini hayo

Alisema kuwa kutokana na mwelekeo wa sasa teknolojia, zinahitaji aina mbalimbali za madini mkakati na kwamba, nchini Tanzania madini hayo yanapatikana kwa wingi.

“Ndugu Washiriki, mengi ya madini mkakati yanayohitajika kwa mabadiliko ya nishati safi yanapatikana kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania. Hizi ni pamoja na rasilimali muhimu ya Grafiti, Nikeli, Kobalti, Lithiamu, Vipengee Adimu vya Dunia (Rare Earth Elements [REE]), Shaba, Manganese, Zinki na Alumini.” alisema Dkt. Kiruswa.

Aidha, Dkt. Kiruswa alisema kuwa kutokana na uwepo wa rasilimali hizo Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu katika Mkakati wa Mpito wa Nishati Safi kutokana na kuwa na Rasilimali Madini muhimu na Mkakati ya aina mbalimbali kwa kiasi kikubwa.

Sambamba na hilo, Dkt. Kiruswa aliueleza mkutano huo kuwa, miongoni mwa masuala yanayohitaji mkakati wa pamoja wa kimataifa, ni pamoja na namna bora ya ugavi wa madini hayo, uboreshaji wa uwazi wa masoko, kuongeza kasi ya teknolojia za uvumbuzi na uchakataji na kukuza mazoea ya maendeleo endelevu na yenye uwajibikaji.

Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini na kuongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo zina amani na utulivu mkubwa kisiasa.

“Tanzania imeunganishwa vyema na mitandao mizuri ya barabara inayofanya mikoa na wilaya zote kufikika. Faida nyingine kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa mfumo ujao wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ambao unaendelea kujengwa kuanzia Bandari ya Dar es salaam hadi katika nchi jirani zisizo na bandari zikiwemo Rwanda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)” aliongeza Dkt. Kiruswa.

Mbali na Naibu Waziri, wengine walioshiriki kutoka Wizara ya Madini ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Uendelezaji Migodi kutoka Wizara ya Madini, Terence Ngole, Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) Hafsa Seif.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mawaziri, Wafanyabiashara, Wawekezaji, taasisi za kimataifa na taasisi za kiraia kutoka nchi tofauti Ulimwenguni.

Katika hatua nyingine Ujumbe huo wa Tanzania ulipata nafasi ya kuzungumza na wadau wengine wa Sekta ya Madini kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India ambapo ulizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kabir ambayo ni sehemu ya Shirika la Madini la Taifa Nchini India, lengo likiwa ni kuona namna nzuri ya kuanzisha ushirikiano wa kikazi na kubadilishana ujuzi kwenye Sekta ya Madini.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania