TANZANIA

Tanzania Kuboresha Mazingira ya Fursa za Makampuni

AGOSTI 24, 2023
Border
news image

Serikali imeweka mikakati na inaboresha mazingira ya kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa mbalimbali nchini ikiwemo za miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipomwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kufunga Kongamano la Wanawake na Manunuzi ya Umma na fursa za biashara katika Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania lililofanyika mkoani Tanga Agosti 24, 2023.

Waziri Dkt. Gwajima amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa fursa zote zinatumiwa na Watanzania hususan Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.

Amefafanua kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili Watanzania katika kushiriki kwenye miradi mikubwa ili kuhakikisha wanashiriki kwa wingi katika fursa za utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

"Ninafahamu kwamba wengi wenu kama watu binafsi lakini pia kama sehemu ya sekta binafsi mnakabiliwa na changamoto mbalimbali kwenye kushiriki utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ukosefu wa mitaji, kutokidhi vigezo na viwango vya kimataifa, ukosefu wa taarifa kamili na sahihi kuhusu mahitaji ya wakandarasi na wawekezaji, pamoja na ukosefu wa ujuzi na uzoefu katika kusimamia fedha na miradi mikubwa." amesema Dkt. Gwajima.

Akizungumzia fursa katika mradi wa bomba la mafuta wa EACOP unaotekelezwa kati ya Kampuni binafsi na Serikali kutoka Hoima -Tanga, Waziri Dkt. Gwajima amesema Mradi huo unatarajiwa kuwa na urefu wa Kms 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania ambapo Kms zaidi ya 200 zitajengwa ndani ya Mkoa wa Tanga na itagharimu Dola za Marekani bilioni 3.55.

"Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuzalisha ajira kati ya 6,000 na 10,000. Hivyo mtaona wazi fursa iliyopo ambayo kiukweli hakuna budi kuitumia kwa ajili ya kukuza uchumi wa familia zenu na Taifa letu kwa ujumla." amebainisha Dkt. Gwajima.

Ameongeza kwamba Mradi huo ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo Serikali imehakikisha wananchi wanashiriki siyo tu katika ajira Bali na shughuli mbalimbali.

Aidha,Dkt. Gwajima amewaahidi wanawake wote kuwa watashirikiana na Wadau wa Sekta zote za Serikali na Sekta binafsi ikiwemo Taasisi ya Ng'arisha Maisha iliyoandaa Kongamano hilo, kutekeleza maelekezo yote ya Serikali. Amewahimiza pia wanawake nchini kote kujiunga na Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Ili kupata fursa ya kufahamu mambo mengi ambayo Serikali inafanya kwenye uwezeshaji.

Halikadhalika Dkt. Gwajima ametoa maelekezo ya Serikali kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Watanzania hususan Wanawake wapewe kipaumbele katika ajira na manunuzi ya umma na fursa za biashara katika miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa nchini kwa kuzingatia ujuzi walio nao na bidhaa na huduma zinazokidhi viwango.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania