TANZANIA

Serikali ya Tanzania Kutafuta Fursa za Kiuchumi kwa Machinga

AGOSTI 26, 2023
Border
news image

Serikali ya Tanzania imejidhatiti kuhakikisha inawainua kiuchumi wafanya biashara ndogondogo kupitia juhudi mbalimbali ikiwemo masharti rahisi ya mikopo kutoka benki mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania, Dkt. Nandera Mhando alipokua akizungumza na Viongozi wa Machinga wa Mikoa juu ya maoni ya utaratibu wa kupata Mikopo kupitia Benki Agosti 26,2023,Jijini Dodoma.

“Ni ukweli usiopingika kuwa juhudi mbalimbali zimechukuliwa na Serikali kupitia Wizara, Wizara za kisekta na Wadau mbalimbali kuhakikisha wafanya biashara ndogondogo wananufaika na fursa za kiuchumi na kupitia kikao hiki Serikali inatarajia kupokea maoni yenu kwani ni kundi kubwa la wawakilishi kutoka mikoa yote.”Alisema Dkt Nandera

Kikao hicho kina lengo la kujadili maeneo makuu matatu ambayo ni Mikopo ya benki kwa wafanyabiashara ndogondogo, Maendeleo ya Mfumo wa kusajili wafanya biashara ndogondogo pamoja na utawala bora na uwajibikaji kwa viongozi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kitengo cha Makundi Maalum, Juma Samuel ametoa wito kwa viongozi hao kuhakikisha wanatoa elimu kwa Machinga kwenye mikoa yao ili waweze kutambua jukumu lao ipasavyo na kupata faida ya mikopo hiyo

“Elimu na uelewa wa masharti ya Mikopo hii ni muhimu sana kwani Itakua ngumu mikopo hii kuwa na tija bila mipango thabiti kwani itakuwa rahisi kwa wafanya biashara wadogo wadogo kushindwa kuitumia mikopo hii na kupelekea utimilifu wa msemo wa “kukopa ni harusi,Kulipa ni Matanga”Alisema Mkurugenzi Juma.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdulnuru amewapongeza kwa kuzingatia jinsia katika uongozi wao kwani Maendeleo yanahitaji ushirikishwaji wa jinsi zote .

Kwa niaba ya Viongozi wote,Mwenyekiti wa Machinga Tanzania Ernest Matondo ameishukuru Serikali kwa juhudi zao za kuhakikisha wanawatengenezea mazingira salama na rafiki ya wao kufanya kazi zao kwani kuinua kundi hili ni kuinua uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania