Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na kuendeleza biashara zao.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima alipokuwa akizindua Programu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ijulikanayo kama Women Empowerment Program (WEP) inayosimamiwa na kuratibiwa na Benki ya EXIM Tanzania, katika hafla iliyofanyika jijini Dar Es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima amesema uchumi unapoimarika ndivyo familia inakuwa na ustawi bora na kupunguza madhira ya vitendo vya ukatili kwenye familia.
“Kwa takwimu tulizonazo, takriban asilimia 70 ya wanawake bado wapo kwenye ajira zisizo rasmi wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo kama mama ntilie na kazi za nyumbani. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu za Finscope za mwaka 2017, kati ya watu 3,014,106 waliokuwa kwenye ajira rasmi, wanawake walikuwa 1,107,917 sawa na asilimia 36.8 tu.” Alisema Waziri Dkt. Gwajima
“Ni matumaini yangu kuwa programu hii ya WEP ya Benki ya Exim imekuja muda muafaka na itakuwa chachu ya kupunguza pengo ili na kuwafanya wanawake washiriki kikamilifu katika sekta ya kifedha” alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima ameipongeza Benki ya Exim Tanzania kupitia mpango huo, kwa kutoa mkopo bila riba wa dola elfu kumi (takribani shilingi milioni 25) kwa wahitimu watatu bora kwa kipindi cha miaka mitatu na kusema jitihada hizo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Akieleza juhudi za Serikali juu ya kuwawezesha wananchi hasa wanawake kiuchumi Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali imeanzisha jumla ya Mifuko 61 ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na hadi sasa imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.22 kwa wanawake millioni 5.3 na mwaka 2018, Serikali ilipitisha sheria ambayo ilizielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba (Wanawake 4%, Vijana 4% na Watu wenye Ulemavu 2%).
“Tangu kipindi hicho, mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 63.489 imetolewa na kuwanufaisha wanawake zaidi ya 938,800.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Jaffari Matundu amesema Benki hiyo imefanikiwa kushirikiana na wadau wengine katika kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za kupata mikopo isiyo na riba ambayo imewasaidia kupata mitaji na kuongeza vifaa vya uzalishaji hivyo kuongeza masoko kwa ajili ya bidhaa zao.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Ndoto Hub, Faraja Nyarandu amesema kuwa mpaka sasa kwa kushirikiana na Benki ya Exim wameweza kuwafikia wanawake 63,000 katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kuendeleza ndoto za biashara zao kwa kupata mitaji na masoko ili kupata mafanikio katika biashara zao.