Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi wameonesha kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na ujio wake katika Wilaya hiyo umewapa faraja.
Wakazi hao wakizungumza katika nyakati tofauti leo wilayani hapo wamesema kuwa Serikali imeboresha maisha yao kwa kuwafikishia huduma mbalimbali.
Mkazi wa Kilimahewa Wilaya ya Ruangwa, Bi. Rahma Hokororo amesema kuwa ziara ya Rais Samia katika Wilaya Ruangwa inawapa matumaini kuwa miradi mingi zaidi ya maendeleo itatekelezwa kwa manufaa yao.
Pia, amemshauri Mhe. Rais Samia kuendelea kufanya kazi na kwa kuwa wao wanaunga mkono jitihada zake za kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa nchini.
" Tunayaona maendeleo kwa macho sio kusimuliwa kwa kweli ana jitihada sana katika kutusaidia Watanzania. Kama mwanamke ameonesha jitihada kubwa sana, siku za nyuma tuliambiwa wanawake hatuwezi chochote lakini yeye ameonesha wanawake tunaweza, Watanzania tuendelee kumuamini Mhe. Rais", amesema Bi. Rahma.
Mkazi wa Mtaa wa Likangala na mjasiriamali, Bi. Zainab Ajibu, amesema kuwa Ruangwa kuna umeme wa uhakika na barabara zinaendelea kujengwa hivyo wananchi hao wanapongeza jitihada hizo za Serikali.
" Mfano kuna maji, umeme na mradi wa madini unatekelezwa katika vijiji vya Namikulo, Mihewe na Matambalale, mradi huu unasaidia vijana kupata ajira za muda mfupi na lakini na kupata fedha za kuhudumia familia zao", amebainisha Bi. Ajibu.
Aidha, amesema kuwa huduma za afya ikiwemo za uzazi zimeendelea kuimarika na kupatikana kwa urahisi na haraka wilayani humo.
Pia, Bw. Abubakar Mkwepu amesema kuwa waanamini ujio wa Mhe. Rais utawapa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajasiriamali kuuza bidhaa zao na wengine kuona fursa za uwekezaji zilizopo wilayani humo.
" Baadhi ya miradi imekamikika, mfano Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, pia kuna vituo vya afya ikiwemo cha Mbuyuni vimekamilika na tayari vimeanza kutoa huduma kwa kweli tunampongeza na kumshukuru Rais Samia", ameeleza Bw. Mkwepu.
Ameongeza kuwa katika miradi ya elimu, kuna majengo ya kisasa katika kila kijiji na wanafunzi wasoma katika mazingira bora.
Mhe. Rais Samia ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Lindi ambapo ataweka mawe ya msingi na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Shule ya Sekondari ya Wasichana Lindi, Bandari ya Uvuvi sambamba na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.