Waganga wakuu wa Mikoa nchini Tanzania wametakiwa kuwajibika katika majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miiko ya taaluma zao ili kuendelea kutoa Huduma bora kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Wasilimali Watu - Wizara ya Afya Dkt. Saitori Laizer wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu kwenye kikao cha baraza la madaktari na waganga wakuu wa Mikoa kilichofanyika Mkoani Dodoma.
“Waganga Wakuu wa Mikoa mnatakiwa kuwasimamia vyema watumishi wote wazingatie sheria na miiko kwani yeyote atakaekutwa na hatia ya kuvunja sheria au taratibu na miiko ya taaluma hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa”. Amesema Dkt. Saitori
Aidha, Dkt. Saitori amewataka Waganga hao kusimamia ubora wa Huduma za Afya na usalama wa wananchi wanapofika katika vituo vya kutolea Huduma hizo ili wapate huduma bora na kwa wakati.
“Mnazo kamati na mifumo ambayo iko katika Mikoa na Halmashauri zenu ambazo zinawaelekeza ikatumike vizuri katika kusimamia taaluma na ubora wa Huduma na usalama wa wananchi wakiwa katika vituo vya kutolea Huduma za afya”. Amesisitiza Dkt. Saitori
Hata hivyo Dkt. Saitori amesema Wizara ya Afya inapokea maamizio ya kikao hicho katika kuendelea kutoa Huduma bora kwa wananchi ili wawe na Afya njema na kuendelea kufanya shughuli za kimaendeleo nchini.
“Tupo tayari kupokea maazimio yenu ambayo yatakuwa tija kwa Taaluma yenu na hasa kumsaidia mwananchi kupata huduma bora na kwa wakati”. Amesema Dkt. Saitori