TANZANIA

Rc Senyamule Akerwa Na Wizi Wa Vifaa Vya Ujenzi

OKTOBA 03, 2023
Border
news image

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amebaini wizi wa vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko kumi (10) ya Saruji katika Shule ya Wasichana mpya ya Sekondari ya Mkoa wa Dodoma inayojengwa katika Kata ya Manchali Wilayani Chamwino Mkoani humo.

Senyamule amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na kutoa maelekezo kwa mafundi wanaotekeleza ujenzi huo washule hiyo

"Hapa jana imekamatwa mifuko kumi ya simenti iliyokuwa imebebwa na boda boda wawili kila mmoja mitano lakini hatujui ilikusudiwa mingapi kuchukuliwa na hapa kwetu sisi haijalishi ni mfuko mmoja au mitano au mia moja kwetu sisi inathamani kwa sasabu itapelekea kuharibika kwa ubora wa kazi kwa kile ambacho kimekusudiwa" ameeleza Senyamule

Aidha, Mhe. Senyamule ameagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote wanahusika na wizi huo ili iwe fundisho kwa wengine.

"Sasa nitoe agizo kwa kuwa na pamoja wahalifu wameshikwa tupate taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwa wote waliohusika haijalishi awe na cheo gani hakikisheni wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine "ameagiza Mhe.Senyamule

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Msuya amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa watahakikisha wote walioshiriki kwenye wizi huo wanachukuliwa hatua kali za kisheria .

Nae, Afisa Tarafa wa Chilonwa Bw. Japhari Kikoti kwa niaba ya Mkurugenzi wa Chamwino Dkt. Semastatus Mashimba amesema lengo ni kukamilisha mradi kwa wakati hivyo watahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati bila kusuasua.

Ujenzi wa Shule hiyo ya Wasichana ya Chamwino unagharimu kiasi cha shillingi Bilioni Tatu ambapo unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania