TANZANIA

NIRC Mbioni Kujenga Bwawa La Umwagiliaji Skimu Ya Dakawa Kwa Lengo La Kupanua Eneo La Umwagiliaji

SEPTEMBA 18, 2023
Border
news image

Wakulima skimu ya Ushirika wa Wakulima Wadogo wadogo kilimo cha mpunga Dakawa (UWAWAKUDA)wameishukuru Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Tanzania kwa kuwapatia elimu ya umuhimu wa uchangiaji ada ya huduma za umwagiliaji na usajili wa vyama vya umwagiliaji.

Hayo yanajiri katika mkutano wa kawaida wa mwaka wa chama cha ushirika cha wakulima wa Umwagiliaji skimu ya Dakawa wilayani Mvomero mkoani Morogoro,ambapo mkutano huo ulihudhuriwa na wataalamu wa Tume ya Taifa Umwagiliaji makao makuu,pamoja na wataalamu ofisi ya Tume mkoa wa Morogoro.

Wakulima hao wameeleza kuwa, awali walikuwa na uelewa mdogo juu ya sheria ya taifa ya umwagiliaji inayomtaka mkulima kuchangia ada ya huduma za umwagiliaji na kusajili chama chini ya Tume ya Umwagiliaji, hivyo ujio wa wataalamu hao umewasaidia kuwa na uelewa wa umuhimu wa zoezi hilo kwa manufaa ya sekta ya umwagiliaji nchini.

Akizungumza mara baada ya kutoa elimu kwa wakulima hao, afisa kilimo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutoka makao makuu, na ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu,Bw. Petro Sarwat ameeleza umuhimu wa uchangiaji ada ya huduma za umwagiliaji na kwamba ada hiyo itasaidia kuboresha na kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji nchini.

" Moja kati ya vipengele ambavyo tunawaelimisha wakulima wetu waelewe kwamba miundombinu iliyopo ni ya kwao lakini pia wachangie ili serikali iweze kufikia malengo yake, kwani kwa sasa eneo linalofaa kwa umwagiliaji kwa nchi nzima ni hekta milioni 29 na eneo lililoendelezwa ni hekta 727,280,hivyo serikali ina majukumu na wakulima wana wajibu wa kuchangia ili serikali iweze kuboresha miundombinu iliyopo na kuiendeleza"

Kwa upande wake Mhandisi Umwagiliaji mkoa wa Morogoro Bw. Mohammed Mcheni,alibainisha kuwa skimu ya Dakawa ni miongoni mwa skimu kubwa katika mkoa huo ambapo takribani bilioni 23.4 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambapo uzalishaji wake ni zaidi ya gunia 20 kwa ekari moja, hivyo serikali kuwekeza katika eneo hilo inaongeza usalama wa chakula kwa mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla.

“Eneo hili la Dakawa zipo hekta 1,000 ambazo hazijaendelezwa na zipo kwenye mpango wa mwaka huu wa fedha kufanya upembuzi yakinifu wa kina pamoja na kufanyia usanifu na tutazijenga hizo ambapo kukamika kwake kutakuwa na takribani hekari 8,000 ambazo zitatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kwahiyo serikali imedhamiria kuendeleza skimu ya Dakawa kwani ni eneo lenye uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula cha kutosha"

Kwa upande wake afisa sheria Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bi. Magreth Shayo, ametoa wito kwa wakulima wa skimu ya Dakawa na wakulima wote nchini kuwa wakulima wapo katika mikono salama ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kwani utekelezaji zoezi la uchangiaji ada ya huduma za umwagiliaji ni kwa mujibu wa wa sheria na ina manufaa kwa wakulima hivyo itasaidia kukuza sekta ya umwagiliaji nchini.

Skimu ya Dakawa ni skimu yenye ukubwa hekari 5016, ambapo serikali ipo mbioni kutekeleza mradi wa ujenzi bwala la umwagiliaji, ambalo litaongeza maji katika skimu hiyo ili kukabiliana na upungufu wa maji katika skimu hiyo na kuongeza uzalshaji wenye tija kwa wakulima wa Dakawa hivyo kuwa na uhakika wa chakula.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania