TANZANIA

NCAA Kufungua Malango Mapya Mawili Ya Kuingia Hifadhi Ya Ngorongoro

SEPTEMBA 21, 2023
Border
news image

Katika uboreshaji wa huduma kwa watalii wanaongia ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inatarajia kufungua malango mawili mapya katika eneo la Engaruka na Eyasi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu kamishna wa NCAA (Uhifadhi, utalii na maendeleo ya Jamii) Elibariki Bajuta wakati wa ziara ya Viongozi Chama cha waongoza utalii Tanzania (TTGA) waliotembelea hifadhi ya Ngorongoro.

Bajuta ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuboresha huduma kwa wageni wanaongia ndani ya hifadhi, kuongeza mtawanyiko kwenye vivutio vya utalii na kupunguza msongamano wa wageni katika geti la Loduare na barabara kuu ya Loduare, Seneto hadi Golini ambapo ni mpakani mwa hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.

Naibu Kamishna Bajuta amebainisha maeneo yatakayojengwa malango hayo kuwa ni eneo la Eyasi ambapo ujenzi wa lango umekamilika na kazi zinazoendelea ni kusimika mifumo ya malipo na mtandao wa intaneti sambamba na uboreshaji wa barabara ya kutoka eyasi kupitia mlima Endulen, Ndutu hadi uelekeo wa Serengeti ili wageni wanaokuwa eneo la ziwa Eyasi kwa shughuli za utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) wasilazimike kurudi karatu na kuingilia geti la Loduare kwenda Ngorongoro.

Lango la pili litajengwa mpakani mwa eneo la Engaruka na Empakaai kreta na ujenzi huo utaenda sambamba na kufungua barabara itakayoanzia Engaruka kuelekea kreta za empakaai, olmoti kreta, mlima lolmalasin hadi kreta ya Ngorongoro.

“Ujenzi huu unalenga kupanua wigo wa huduma kwa wageni ili watawanyike kwenye vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi, geti la mpakani mwa Empakaai na Engaruka litakapokamilika wageni wanaoenda kutalii eneo la ziwa Natron hawatalazimika kurudi mto Wambu hadi karatu ili waingie hifadhi ya Ngorongoro” ameongeza Bajuta.

Amebainisha kuwa ujenzi wa malango hayo utaanza katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 na kukamilika mwaka ujao wa fedha 2024/2025.

Sambamba na ujenzi wa malango hayo Serikali kupitia NCAA iliweka mkandarasi wa kukarabati barabara kutoka eneo la View Point hadi Nayobi yenye urefu wa kilomita 78 ambayo tayari imeshakamilika na kusaidia ongezeko la watalii kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko mashariki mwa hifadhi Ngorongoro ambavyo ni, empakaai Kreta, Olmoti Kreta, Mlima Lolmalasin na maeneo ya nyanda za juu kaskazini.

Aidha katika kuongeza mtawanyiko wa watalii ndani ya Hifadhi, NCAA inaendelea na ujenzi wa barabara mpya ya kiwango cha changarawe kutoka enduleni hadi ndutu yenye urefu wa kilomita 45, hadi sasa kilomita 20 zimekamilika na kilomita 25 zilizobaki mkandarasi anaendeleo na ujenzi.

Barabara hii inayopita eneo la ndutu ambalo ni maarufu kwa mazalia ya Wanyama wanaohama (Nyumbu) itakapokamilika, wageni watapata fursa ya kupitia Endulen, Ndutu hadi mpakani mwa hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti bila kupita barabara kuu ya Loduare, Seneto, Golini, Serengeti.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania