TANZANIA

Naibu Waziri Mkuu Aielekeza REA Kutumia Muda Mwingi Vijijini Tanzania

SEPTEMBA 20, 2023
Border
news image

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini Tanzania Dkt.Doto Biteko ameiagiza Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini nchini Tanzania (REA)kutumia muda mwingi zaidi wa kazi vijijini na muda mchache ofisini ili waendelee kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Ameyasema hayo baada ya kukutana na kuzungumza na Menejimenti ya REA katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati, zilizoko jijini Dar es Salaam.

“Najua mnafanya kazi kubwa ya kuandaa na kuratibu miradi mnayoitekeleza lakini nawashauri nendeni vijijini na tumieni muda mwingi zaidi wa kazi vijijini ambako ndiko miradi yenu inakotekelezwa ili muweze kuisimamia vizuri na kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi,” amesisitiza.

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza REA kwa kazi nzuri inayofanya katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za nishati bora sawa na walioko mijini. Amewataka kuendelea kuchapa kazi ili azma ya Serikali kuhakikisha kila mwananchi aliyeko kijijini anatumia nishati bora iweze kufikiwa.

Awali, akiwasilisha taarifa za miradi inayotekelezwa, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kutoka asilimia mbili wakati Wakala unaanzishwa mwaka 2007 hadi asilimia 69 mwaka 2020.

Mhandisi Saidy amesema kuwa mafanikio mengine ni kuwezesha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Makao Makuu ya Wilaya 26 ambayo yalikuwa hayajafikiwa pamoja na kuanzisha mpango wa kupeleka umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara.

“Hadi Agosti 31 mwaka huu jumla ya vijiji 10,987 sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote vimefikiwa na umeme na vilivyobaki vitakamilika kabla ya Juni 2024,” ameeleza.

Vilevile, ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuunga vijiji na vitongoji 4, 234 kwa kipindi cha miaka miwili kupitia miradi mbalimbali, kusaini mikataba ya miradi sita kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita pamoja na kuwezesha ujenzi wa miradi midogo 121 hivyo kuunganisha wateja 178,401 katika maeneo mbalimbali yaliyo mbali na gridi ya Taifa.

Mengine ni kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi wa miradi kutoka viwanda sita mwaka 2007 hadi viwanda 56 mwaka 2021 ambavyo huzalisha nguzo, nyaya, mita, mashineumba na viunganishi.

Mkurugenzi Mkuu amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, REA itaendelea kujituma pamoja na kuleta ubunifu katika kuharakisha upatikanaji wa nishati bora maeneo ya vijijini.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania