TANZANIA

Mameneja wa TARURA Tanzania Waagizwa Kusimamia Kikamilifu Mradi wa TACTIC

SEPTEMBA 5, 2023
Border
news image

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI nchini Tanzania Dkt. Festo J. Dugange(Mb) amewaagiza Mameneja TARURA wa Mikoa na Wilaya zote nchini zinazotekeleza Mradi wa kuboresha miundombinu katika Majiji, Manispaa na Miji (TACTIC) kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu hatua zote za manunuzi na kuhakikisha Wakandarasa wanafika katika maeneo ya kazi kuanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema hayo leo Bugeni Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Mashaka Gambo aliyetaka kujua Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa kwenye eneo la Bondeni City Jijini Arusha kupitia Mradi wa TACTIC.

Dkt. Dugange amesema Serikali kupitia Mradi wa TACTIC itatekeleza ujenzi wa stendi kuu ya kisasa ya mabasi, Masoko mawili pamoja na Bustani moja ya mapumziko kwenye eneo la Bondeni City kwa lengo la kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani.

Dkt. Dugange ameeleza kuwa Utekelezaji wa mradi wa TACTIC, kazi ya usanifu imekamilika na taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata mzabuni inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2023, baada ya taratibu hizo kukamilika, utekelezaji wa ujenzi kwenye maeneo yaliyoainishwa utaanza.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania