TANZANIA

Maafisa Ugavi Tanzania Watakiwa Kuzingatia Ukomo Wa Vifaa Vinavyomomonyoa Tabaka La Ozoni

AGOSTI 25, 2023
Border
news image

Serikali ya Tanzania imewataka maafisa ununuzi na ugavi kuzingatia ukomo wa matumizi ya kemikali na vifaa vyenye kemikali ambazo zinamong’onyoa tabaka la ozoni au kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Agosti 25, 2023 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa Maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Dkt. Mkama amesema mwanzoni mwa miaka ya 1970, wanasayansi walibaini baadhi ya kemikali zinazotengenezwa na binadamu ikiwemo majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto na utengenezaji wa magodoro vimejipenyeza angani na kumong'onyoa tabaka la hewa ya Ozoni na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Matokeo ya kumong’onyoka kwa Tabaka la Ozoni ni kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo husababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira. Madhara hayo ni kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho unaosababisha upofu na athari kwa kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine” amesema Dkt. Mkama

Aidha Dkt. Mkama amesema matokeo ya uvumbuzi huo yalisababisha Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mazingira (UN Environment) kufanya tathmini ya kisayansi na kuamua kuchukua hatua madhubuti kulinda tabaka la Ozoni kwa kuanzisha Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la Ozoni iliyopitishwa mwaka 1987.

Akifafanua zaidi Dkt. Mkama amesema katika kutekeleza Itifaki hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kuondosha Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni Jamii ya Hydrochlorofluorocarbons (HCFCs) ifikapo mwaka 2030 pamoja na Mpango wa utekelezaji wa Marekebisho ya Kigali ya kupunguza matumizi ya kemikali jamii ya hidrofluorokaboni.

“Chini ya Mipango hii mojawapo ya shughuli zinazotelekezwa na zinazopaswa kutekelezwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kutoka katika Taasisi mbalimbali kukusu utekelezaji wa Itifaki husika ikiwemo utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni) za mwaka 2022” amesema Dkt. Mkama.

Dkt. Mkama amesema maafisa ununuzi na ugavi ni wahusika wakuu katika mchakato wa wa kushugulikia manunuzi ya vifaa mbalimbali katika ofisi za umma, hivyo wana wajibu mkubwa wa kutoa elimu ya Ozoni kwa wengine ili kuongeza juhudi za kuhifadhi Tabaka la Ozoni na kuokoa Maisha ya binadamu na viumbe hai.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema katika kutekeleza Itifaki hiyo, Ofisi hiyo imeendelea kutoa mafunzo wa wadau mbalimbali wakiwemo maafisa ununuzi na ugavi kutoka katika Wizara mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu matakwa ya Itifaki ya Montreal.

“Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania na Vyuo mbalimbali vya Mafunzo ya Ufundi tumeendelea kutoa mafunzo kwa maafisa mbalimbali kuhusu usimamizi na udhibiti wa kemikali na vifaa vyenye kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki hii” amesema Kemilembe.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania