TANZANIA

'Kustaafu Sio Kuchoka' - Mhe. Senyamule

OKTOBA 02, 2023
Border
news image

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania Mhe.Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wastaafu watarajiwa kuendelea kutumia ujuzi wao kwakuwa wanamaarifa na uzoefu hivyo kuhakikisha wanajiunga katika taasisi zingine kwani Taifa bado linawahitaji.

Kadhalika, amewaalika kuwekeza Mkoa wa Dodoma kwani ndio Makao Makuu ya nchi hivyo bado kuna fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo miundombinu mbalimbali kama vile Hoteli ,Kilimo na Utalii.

Mhe.Senyamule ametoa wito huo wakati akifunga semina ya wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) iliyofanyika kwa muda wa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano Jengo la PSSSF Jijini Dodoma.

"Kustaafu siyo kuchoka nikiwaangalia hapa sioni hata mmoja ambaye anaonekana kuchoka hivyo wekeni juhudi na maarifa pia tumieni uzoefu wenu katika taasisi nyingine za binafsi kwani muda baada wa serikali kuisha "Amesisitiza Senyamule

Mhe.Senyamule amesema lengo la semina hiyo ni kuwaandaa na kuwaelimisha juu ya maisha baada ya kustaafu kwani watu ambao bado wapo kwenye utumishi wanajivunia wastaafu ikiwa wengi wao wamelitumikia taifa kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Katika Hatua nyingine, Mkuu Mkoa huyo amemshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uthubutu wake wa kuamua kulipa deni la shilingi trilioni 4.6 la wanachama wa uliyokuwa Mfuko wa PSPF ya kabla ya 1999 uamuzi huo umewezesha PSSSF kulipwa kiasi cha shilingi trilioni 2.17 kupitia hatifungani maalumu.

"Serikali pia imelipa shilingi bilioni 500 katika deni la shilingi bilioni 731.4 la Mikopo ya miradi ambayo mifuko iliyounganishwa iliikopesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali kama vile Jengo la Bunge, Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo ,Nelson Mandela Institute of Science and Technology na Chuo Kikuu cha Dodoma. "Amesema Senyamule

Sanjari na Hilo, Mhe.Senyamule amewaasa wastaafu watarajiwa kujihadhari na matapeli wa mitandao ya kijamii kwani tayari wanaelimu kuhusu viashiria vya meseji ya matapeli .

Nae,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bi.Beatrice Lupi amesema semina hiyo ni Muhimu kwa mustakali wa Wastaafu na Taifa kwa ujumla kwani moja ya majukumu yao ni kutambua wanachama ,kuwasajiri na kutunza kumbukumbu sambamba na kutoa elimu zinazohusu wanachama ,waajiri na mafao ,ili kuhakikisha wanapoondoka kwenye utumishi wanakuwa na uhakika wa maisha baada ya Kustaafu.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023 /2024 wanatarijia kuwa na wastaafu 11,000 idadi hiyo inategemewa kuongezeka kila mwaka.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania