TANZANIA

Kinana: Tamasha La Kizimkazi Chachu Kuimarisha Muungano

AGOSTI 31, 2023
Border
news image

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara), Ndugu Abdulrahman Kinana, amesema Tamasha la Kizimkazi limefanikiwa kuwa chachu ya kuimarisha Muungano.

Kinana amesema hayo Agosti 31, 2023, alipozungumza kwenye Tamasha la Nane la Kizimkazi, Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti amesema, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa nchi, amedhirisha uongozi ni kuonyesha njia katika nyanja zote.

"Nchi yetu imepata maendeleo makubwa katika nyanja zote,” alisema Ndugu Kinana katika tamasha hilo lililopambwa na kazi za utamaduni, sanaa na kuhudhuriwa na halaiki ya watu.

Ndugu Kinana alisema, kwa ukubwa na umaarufu wa tamasha hilo, siyo shughuli ya Zanzibar tu, bali ni tukio ambalo limeweka misingi mizuri ya kuimarisha Muungano.

Amefafanua kwamba, tamasha hilo kwa mwaka huu limewavuta Watanzania wengi kutoka nje ya Zanzibar kushiriki, na siku zijazo wengi zaidi watamiminika Kizimkazi siyo tu kujionea bali kushiriki.

Ameongeza kusema kuwa, kuna matamasha mengi, katika nchi mbalimbali na kutoa mfano wa Brazil, Italia,  India,  Uhispania na Ireland; na kwa namna Tamasha la Kizimkazi lilivyofana, linaelekea kuwa la viwango vya kimataifa .

 "Shughuli hii nadhani imeanza kama miaka mitatu hivi, lakini kwa namna tunavyoiona, itakuja kuwa ya kimataifa, itaingia kwenye kalenda ya dunia na watu wote duniani watapanga tarehe za kuja Kizimkazi," alisema Ndugu Kinana.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania