TANZANIA

Kazi Ya Mtumishi Wa Umma Tanzania Ni Kutatua Kero Za Wananchi - Dkt. Jingu

SEPTEMBA 5, 2023
Border
news image

Katibu Mkuu Wizara ya Afya nchini Tanzania Dkt. John Jingu amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuunganisha mawazo na nguvu zao ili kutatua kero za wananchi kwa kutoa huduma bora.

Dkt. Jingu ameyasema hayo mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, na kupokelewa na Menejimenti na Watumishi wa Wizara wakiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumanini Nagu.

“Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, sisi wote hapa tuna uwezo mbalimbali, nina uhakika tukiunganisha mawazo yetu pamoja tutajua namna gani tufanye ili tuweze kutatua kero za wananchi”, amesema Dkt. Jingu

Aidha, Dkt. Jingu amewataka watumishi wa Wizara ya Afya kuimarisha mahusiano mazuri kazini kwa kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana ili kutekeleza majukumu vizuri na kumrahisishia yeye kufanya majukumu yake vizuri aliyotumwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tunapokuwa katika mazingira haya ya kazi, ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri ni lazima tuwe na mahusiano mazuri kazini kwa kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana, lakini pia ni amaelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuheshimiana kazini kwa ngazi zote,” amesema Dkt. Jingu

Amesema, eneo la kazi ndio familia namba moja kwa kuwa tunatumia muda wetu mwingi kuwa kazini kuliko katika familia zetu za nyumbani, Mke, Mume na watoto, hivyo ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri lazima kuwe na mahusiano mazuri kazini.

“Hata Kama mnauwezo mkubwa wa kufanya kazi kiasi gani lakini kama hakuna upendo, mahusiano mazuri kazini kuheshimiana, basi hakuna kazi itakayofanyika ikawa nzuri sababu ya kutokuwa na umoja”, amesema Dkt. Jingu

Pia, Dkt. Jingu amewataka watumishi wa Wizara ya Afya hao kuwa na tabia ya kumsikiliza Rais Samia popote anapoongea kwakuwa inawezekana akatoa maagizo yanayoihusu Sekta ya Afya, na kuanza kuyatekeleza kwa haraka.

“Sisi watumishi wa umma lazima tuwe na tabia ya kufatilia popote anapozungumza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kama kuna maagizo anayatoa na yanayohusu Sekta ya Afya basi tuyafanyie kazi kwa haraka sana”, amesema Dkt. Jingu

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania