TANZANIA

Kapinga: Mwanzoni Mwa Oktoba 2023 Tunaanza Kuwalipa Fidia Waliopisha Mradi wa Kituo Kusambaza Umeme cha Uhuru

SEPTEMBA 28, 2023
Border
news image

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaanza kuwalipa fidia ya shilingi milioni 399 kwa wananchi 496 waliopisha Mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Uhuru kilichopo katika Kijiji cha Vumilia Wilayani Urambo Mkoani Tabora.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo hicho kilichopo wilayani Urambo Mkoani Tabora.

Amesema Fedha hizo za fidia zitaanza kulipwa kuanzia mwanzoni mwa mwezi Oktoba ambapo taratibu zote za ulipaji fidia hiyo zimekamilika.

“Wananchi nawaomba muandae nyaraka zote muhimu zikiwepo barua na vitambulisho vinavyothibitisha kulipwa fidia ili tarehe 2 Octoba, 2023 mtakapoanza kulipwa fedha zenu kusitokee changamoto ya aina yeyote itakayochelewesha malipo hayo, fedha ziko tayari na taratibu zote zimekamilika”, alisema Mhe. Kapinga.

Aidha amesema ujenzi wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 66 ya utekelezaji wake unaendelea vizuri.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na mikoa mingine iliyo jirani.

Mradi huyo pia unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Kigoma pamoja na vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme vya Urambo na Nguruka.

Vilevile mradi wa njia ya kusafirisha Umeme kutoka Tabora hadi Katavi, pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kupoza na Kusambaza Umeme vya Ipole, Inyonga na Mpanda.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kapinga, amewasha umeme katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Urambo pamoja na kuzungumza na Wananchi.

Amewasihi wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya umeme kwa kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Kenan Kihongosi ameishukuru Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha upatikaji wa huduma za kijamii ikiwepo, Umeme, Vituo vya Afya, Maji, shule na Barabara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.

Ziara hiyo imehudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Urambo Mama Magreth Sitta, Viongozi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini(REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Naibu amefanya ziara ya siku tatu ya kukagua Maendeleo ya mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika wilaya za Nzega, Uyui na Urambo kwa kuwasha umeme katika baadhi vijiji na kuzungumza na wananchi.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania