Kamati ya kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo nchini Tanzania imeipongeza Wizara ya Kilimo kwa utekelezaji mradi uandaaji mashamba ya mradi wa jenga kesho iliyo bora (BBT) utakaonufaisha zaidi ya vijana mia tano.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo eneo la Ndogowe wilayani Chamwino jijini Dodoma.
Akitoa pongezi hizo mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Mariam Ditopile (Mbunge wa Viti Maalum) mbali na kuipongeza Wizara ya Kilimo katika utekelezaji wake madhubuti, pia ameshauri kuwa watekelezaji wa mradi huo wazingatie kuwanufaisha wenyeji wa eneo hilo la mradi hususani vijana.
Naye mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Kunti Majala (Mbunge wa Viti Maalum) amesema iwapo mradi huo utawashirikisha wenyeji wa vijiji vilivyozunguka mradi huo utasaidia kuepukana na uharibifu wa miundombinu ya mradi huo.
“Ni vyema mkakaa na wenyeji wa eneo hili na mkawashirikisha katika kila hatua kama mlivyowashirikisha wakati wa kuchukua eneo pamoja na mengine yote ili kuepukana na migogoro na uharibifu wa eneo la Mradi”.
Kwa upande wake afisa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Method K. Kihango ambaye ni Afisa Kilimo ameieleza kamati hiyo kuwa zoezi la kusafisha eneo la mradi linaendelea na tayari ekari 4000 zimefanyiwa usafi na kazi bado inaendelea, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi ya vijana wanufaika wa mradi huo ndani ya eneo la mradi.
Bw. Method ameongeza kuwa, uchimbaji wa visima na mabwawa unaendelea na vijana watakapokuja, maji yatakuwepo na shughuli zote zilizopangwa zitaendelea kama zilivyoandaliwa.
Aidha mjumbe wa kamati hiyo ya Bunge, Mhe. Medadi Kalemani (Mbunge wa Chato) amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwekeza fedha kwaajili ya utekelezaji wa mradi wa BBT sambamba na kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa usimamizi thabiti wa utekelezaji wa mradi huo.
Eneo hilo la mradi wa jenga kesho iliyo bora lililopo Ndogowe lina ukubwa wa zaidi ya ekari elfu 11, umelenga kuhudumia vijana zaidi ya 500.