Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini Tanzania Dkt. Doto Biteko amewaeleza watanzania kuwa changamoto ya kukosekana umeme wa uhakika ni ya muda mfupi kwa sababu Ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha umeme wa JNHPP wa Megawati 2,115 umefikia asilimia 91.72 hadi sasa.
Dkt.Biteko amesema hayo wakati wa ziara yake ya kwanza kutembelea mradi huo, tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, iliyofanyika tarehe 16 Septemba, 2023 mkoani Pwani kwa lengo la kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa na wa kielelezo kwa nchi yetu, ambapo Serikali imewekeza fedha nyingi takribani Shilingi trilioni 6.558 ili kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote.
“ Tupo katika hatua za mwisho za ujenzi wa mradi huu ili tuweze kuwapatia watanzania umeme wa uhakika, waweze kukuza uchumi wao, uwepo wa mradi huu tunaamini kwamba changamoto ya umeme tuliyonayo kwa sasa ni ya muda mfupi kwa kuwa ujenzi wa mradi umefikia asilimia 91.72”, amesema Dkt. Biteko
Alifafanua kuwa tayari Serikali imekwishamlipa mkandrasi asilimia 85.5 ya malipo yake ya kazi aliyoifanya katika hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi sasa katika mradi huo.
Amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo mkubwa aliouweka katika kutekeleza mradi huo.
Pia amewapongeza wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi huo, Mshauri wa mradi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huo kwa niaba ya Serikali, kwa hatua kubwa iliyofikiwa.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), Maharage Chande na viongozi wengine kutoka wizarani na TANESCO.