KENYA

Jamii ya kimataifa imeahidi kutoa dola bilioni 23 kwa nchi za Afrika katika juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia-nchi

SEPTEMBA 6, 2023
Border
news image

Jamii ya kimataifa imeahidi kutoa dola bilioni 23 kwa nchi za Afrika katika juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia-nchi.

Rais William Ruto ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa mataifa ya nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia-nchi alitoa hakikisho kuwa bara la Afrika litazingatia maazimio yaliyoafikiwa wakati wa kongamano la Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia-nchi.Kongamano hilo limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kupunguza viwango vya gesi zinazochafua mazingira jinsi ilivyoafikiwa katika mikataba ya Kyoto na Paris.

Kwenye maazimio hayo yaliyosomwa na rais William Ruto, viongozi wa Afrika wamehimiza jamii ya kimataifa kutimiza wajibu wake wa kufadhili hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.Awali,kiongozi wa taifa kwa mara nyingine alitoa wito wa kufanyia mabadiliko mfumo wa taasisi za kifedha ili kutoa mikopo ya riba nafuu kwa mataifa yanayostawi ,ambayo mengi yao yanajumuisha mataifa ya Afrika.

Rais Ruto alisema bara Afrika liko tayari kufanya maamuzi ya busara yatakayoangazia bara hili.Maazimio hayo ya Nairobi yanatarajiwa kuwasilishwa wakati kongamano la mwaka huu la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia-nchi litakaloandaliwa mjini Dubai kuanzia tarehe 30 mwezi Novemba hadi tarehe 12 mwezi Disemba.

AM/MTVNEWS