TANZANIA

Hifadhi Ya Taifa Arusha Mbioni Kuanzisha Zao Jipya La Utalii Wa Kutembelea Maeneo Yenye Mabonde Yaliyopitiwa Na Mito (Canyoning)

SEPTEMBA 21, 2023
Border
news image

Bodi ya wadhamini TANAPA iliyozinduliwa takribani wiki chache zilizopita ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jenerali Mstaafu George Waitara wametembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kufahamishwa kuwa hifadhi hiyo iko mbioni kuanzisha zao jipya la utalii lijulikanalo kama "Canyoning" ili kuongeza idadi ya watalii na kufikia adhma ya serikali ya watalii milioni 5. Ziara hiyo imefanyika katika hifadhi hiyo iliyopo jijini Arusha.

Zao hili jipya la utalii litakuwa ni la kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kuanzishwa katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba, linatarajiwa kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi hiyo. Baadhi ya nchi duniani zenye utalii wa "Canyoning" ni Afrika ya Kusini na nchi ya Croatia inayopatikana katika bara la Asia.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini TANAPA ameipongeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha kwa kubuni mazao mapya ya utalii kama vile Geopark na ujio huu mpya wa "canyoning", mazao haya yataongeza idadi ya watalii na mapato kwa TANAPA na taifa kwa ujumla.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Yustina Kiwango, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha alielezea lengo la uanzishwaji wa "Canyoning" ni mkakati wa TANAPA kubuni mazao mapya na kuongeza mapato kwa shirika na Taifa. Hata hivyo alieleza kuwa "Canyoning" ni utalii wa kutembea katika mito yenye kina kifupi na mabonde, maporomoko ya maji na kuruka katika miamba iliyo chini ya kivuli cha uoto wa asili.

Hifadhi ya Taifa Arusha ni miongoni mwa hifadhi 21 zinazosimamiwa na TANAPA ikisheheni maziwa yaliyo na utajiri wa ndege aina Flamingo pamoja na Kreta ya Ngurudoto iliyojaa Wanyamapori kama twiga, tembo, nyati, Mbega na aina tofauti ya ndege wakaazi na wahamao.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania